
AFRIKA KUSINI: Mchezaji wa zamani wa Simba, Saidi Sinde, ameonya wachezaji wa klabu hiyo kutowadharau wapinzani wao Stellenbosch kutoka Afrika Kusini, akisisitiza kuwa timu hiyo hucheza kwa ubora wa hali ya juu wanapokuwa ugenini.
Akizungumza akiwa nchini Afrika Kusini, Sinde alisema mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayopigwa Aprili 20 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ni fursa ya pekee kwa Simba kujitengenezea mazingira bora ya kusonga mbele.
“Stellenbosch si timu ya kubezwa, hasa wanapokuwa ugenini. Asilimia kubwa ya mafanikio yao hadi kufikia nusu fainali yametokana na ushindi walioupata ugenini. Simba wanapaswa kuwa makini sana, mechi ya nyumbani ni muhimu kushinda kwa mabao mengi,” amesema Sinde.
Akipendekeza mkakati bora wa Simba, Sinde amesisitiza umuhimu wa kufunga mabao matatu au zaidi katika mchezo wa nyumbani ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kabla ya mechi ya marudiano.
“Simba wanatakiwa kuhakikisha wanaondoka na ushindi wa mabao mengi nyumbani, wanapokwenda Afrika Kusini kazi yao iwe ni kukamilisha tu ushindi huo,” ameongeza.
Akizungumzia mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, Sinde amesema Simba haitakuwa mgeni sana kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya Watanzania katika mji huo.
“Kwa kweli Durban ni kama nyumbani kwa Simba. Watanzania wengi wanaishi huko, naamini uwanja utajaa mashabiki wao, hivyo Simba watakuwa na nguvu ya ziada,” amesema.
Kwa ujumla, Sinde amewataka wachezaji wa Simba kutumia kikamilifu faida ya kucheza nyumbani kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kufuzu fainali ya mashindano hayo makubwa.