
SANTOS, Mzimu wa majeraha bado umeendelea kumuandama Staa wa Santos FC na timu ya taifa ya Brazil Neymar jr baada ya kupata tena majeraha katika kipindi cha kwanza cha mchezo wa Ligi kuu ya nchini Brazil (Brazilian Serie A) timu yake ikishinda 2-0 mbele ya Atletico Mineiro usiku wa kuamkia leo.
Neymar alitolewa katika uwanja wa Estádio Urbano Caldeira akitokwa na machozi baada ya kuonekana kupata maumivu makali katika paja lake la kushoto.
Neymar Jr mwenye miaka 33 amekuwa akiandamwa na majereha tangu alipoumia kwenye mechi ya kuwania nafasi ya Kombe la dunia la 2026 mwezi Oktoba mwaka 2023, tangu kipindi hicho amekuwa akipambana kuwa imara japo ubora aliouonesha hapo Santos ulimrejesha tena kwenye timu ya taifa.
Kocha mkuu wa Santos FC Cesar Sampaio aliwaambia waandishi wa habari kuwa bado mapema sana kuzungumzia hali ya Neymar mpaka atakapopata taarifa rasmi ya daktari wa klabu hiyo inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.
“Ni mapema sana kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu Neymar, bado hatuna taarifa ya daktari. Ni hasara kwetu kwa sababu mambo tuliyopanga yalikuwa yakitokea kama tilivyopanga. Limeshatokea kikubwa tumuombee lisiwe jambo la kumuweka nje mda mrefu” amesema kocha Sampaio.




