Aliyefariki miezi mitatu iliyopita kuzikwa wiki ijayo

PARIS: MIPANGO ya mazishi ya mpiga gitaa mkongwe wa Congo Papa Noel Nedule, aliyefariki Novemba mwaka 2024 nchini Ufaransa, bado inaendelea.
Wanafamilia na maafisa wa serikali ya Congo wamekuwa wakifikiria kumzika nyumbani kwao Kinshasa.
Kulingana na wanamuziki mwenzake, Gode Lofombo, kuna uwezekano mkubwa wa mwili wa Papa Noel kurejeshwa Kinshasa wiki ijayo kwa ajili ya mazishi.
Kwa mujibu wa Saturday Nation, Lofombo amethibitisha kufahamishwa na msemaji mkuu wa serikali ya Congo mjini Paris kuhusu mipango ya kusafirisha mwili wa Papa Noel kurudi nyumbani kwao hivi karibuni.
“Licha ya Papa Noel kutumia sehemu kubwa ya kazi yake ya muziki nchini Ufaransa, watu mbalimbali wakiwemo wanamuziki wenzake wanatamani azikwe nyumbani kwao Congo,” Lofombo amesema.
Kuchelewa kuzikwa kwa Papa Noel kunafanana na tukio la mwanamuziki mwenzake wa Congo Lokassa ya Mbongo.
Lokassa ya Mbongo, amefariki nchini Marekani Machi 2023, amezikwa Desemba mwaka huo huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kabla ya kifo chake, Papa Noel alilazwa katika hospitali ya Grigny (Essonne) nchini Ufaransa alikokuwa akiishi na familia yake kwa zaidi ya miaka 30. Mwili wake umelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti huko Grigny, katika jiji la Paris.
Papa Noel atakumbukwa kwa kutumbuiza na vikundi tofauti nchini Congo Brazzaville na Congo Kinshasa wakati wa uhai wake.