Yemi Alade na ‘gundu’ la tuzo za Grammy kujulikana kesho

LOS ANGELES: MWANAMUZIKI maarufu wa Afro-pop kutoka Nigeria Yemi Alade ana historia kubwa katika tuzo za Grammy akiwa ameshirikishwa katika albamu za wanamuziki wenye majina makubwa duniani na umaarufu wake pamoja na nyimbo zake zenye mchanganyiko wa lugha tofauti lakini hajawahi kushinda Grammy.
Alade ameshirikishwa kwenye albamu ya nyota wa Benin na Ufaransa Angelique Kidjo na albamu ya mke wa Jay Z, Beyonce iliyoteuliwa katika tuzo hizo zitakazotolewa kesho katika jiji la Los Angeles.
Februari 2, ina umuhimu mkubwa kwa Yemi Alade kwani inaweza kubadilisha historia yake ya kutopata tuzo hizo na kupata kupitia wimbo wake wa “Kesho” ulioteuliwa kushindania kipengele cha Muziki Bora kutoka Afrika.
Wimbo wa “Kesho” upo kwenye albamu ya sita ya Yemi Alade inayoitwa “Rebel Queen,” albamu ambayo waandaaji wa tuzo hizo wameielezea kuwa ina muimarisha Yemi kuwa “Mama Africa”.
Alade alipata umaarufu kwa mara ya kwanza na wimbo wake wa mwaka 2014 ulioitwa “Johnny,” ambao mwaka wa 2019 ulimfanya kuwa msanii wa kwanza wa kike wa Nigeria kufikisha maoni milioni 100 kwenye YouTube. Pia alirekodi wimbo huo katika lugha ya Kireno, Kiswahili na Kifaransa.
“Paris ni moja ya miji ambayo ilifungua mipaka yake kwa muziki wangu, na nilipenda Kifaransa hata zaidi,” Alade alisema. “Nilitaka kuwasiliana, kwa hivyo niliamua kutengeneza matoleo ya nyimbo zangu (katika lugha zingine). Ndivyo hadithi ya mapenzi na lugha ilianza.”