EPL

Gwiji achomoa betri United

“Fukuzeni wachezaji 8”

MANCHESTER:GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes ametoa maoni makali kuhusu wachezaji ambao klabu hiyo inapaswa kuwaondoa ili kujenga timu imara chini ya kocha Ruben Amorim. Scholes, aliyewakilisha United mara 714 na kufunga mabao 155 na asisti 83 wakati wa enzi yake, ameonya kuwa nyota wengi hawafai kubaki kikosini, huku akiwataka waendelee na juhudi za kuimarisha hali ya kifedha ya klabu hiyo.
Akizungumza na TNT Sports, Scholes alisisitiza kwamba Manchester United inahitaji mageuzi makubwa, huku akitaja majina ya wachezaji wanane kutoka kikosi cha kwanza aliowataja kuondoka. Cha kushangaza, alihimiza klabu iendelee kumvumilia kipa Andre Onana licha ya kukosolewa kwa makosa yake katika mechi dhidi ya Brighton ambapo walifungwa 3-1.
 
Wachezaji Alioorodhesha Kuondolewa ni Matthijs de Ligt,Lisandro Martinez, Luke Shaw,Mason Mount,Antony, Joshua Zirkzee,Casemiro, na Marcus Rashford.
Scholes alimkosoa Luke Shaw kwa kuwa hajakuwa fiti msimu huu, akiichezea timu mara tatu pekee, huku akitoa wito wa kumuuza. Aidha, Scholes alieleza kutoridhishwa kwake na Antony, Zirkzee, na hata Casemiro, akihisi wanapaswa kuondoka ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya.
Kwa upande wa Marcus Rashford, ripoti zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo anataka kuondoka, huku Barcelona na Borussia Dortmund zikihusishwa naye. Hata hivyo, mshahara wake wa £350,000 kwa wiki ni kikwazo kwa miamba hiyo ya Ulaya, ingawa Barca wanapanga kuachana na Eric Garcia na Ansu Fati ili kumpa nafasi Rashford.
Scholes alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Manchester United kuwabakisha vipaji vyao vijana, Kobbie Mainoo na Alejandro Garnacho, akiwataja kama nyota wa siku za usoni. “Itakuwa jambo la kijinga kumuuza Mainoo kwa sababu ya kanuni za kifedha. Amekuwa hapa tangu akiwa na umri wa miaka saba au nane, na ni mchezaji ambaye anaweza kuwa tegemeo kwa miaka 10 ijayo,” alisema.
Hali bado ni tete Old Trafford, na kwa wiki mbili zilizobaki kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho la Januari, mashabiki wanasubiri kuona ni nani ataondoka na nani atabaki katika jitihada za kurejesha heshima ya klabu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button