
KOCHA MKuu wa Ihefu, Juma Mwambusi amesema kama kuna mtu yeyote anayeamini kwamba Ihefu itashuka daraja afute kauli yake kwani anachoamini huo ni upepo mbaya umeikumba timu hiyo.
Akizungumza na Spotileo, kocha huyo amesema kizuri zaidi upepo huo umekuja mwanzoni mwa msimu kwa hiyo kuna muda wa kurekebisha makosa na kufanya vizuri.
Amesema bado kuna vitu vingi vya kubadilisha ndani ya timu hiyo na anachofurahia ni kwamba kile anachofundisha tayari kimeanza kuleta mabadiliko.

“Nimeanza taratibu kubadilisha baadhi ya vitu ambavyo nilidhani ndio vinasababisha ushindi ukosekane. Naamini kadri tunavyokwenda tunazidi kuimarika na ipo siku kuna timu itaacha pointi tatu na hapo tutakuwa tayari kwa mapambano,” amesema Mwambusi.
Kocha huyo amesema sare iliyopata timu yake dhidi ya Tanzania Prisons ni matokeo mazuri ya kazi aliyoianza ya kukijenga kikosi hicho.
Ihefu kwa sasa ina pointi 1 baada ya michezo mitano iliyocheza ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu yenye timu 16.
Mchezo wa Ligi Kuu unaofuta kwa Ihefu utakuwa Oktoba 8 dhidi ya jirani yake Mbeya City.