Ukiiangalia filamu hii hutajutia (The White Tiger)

WALE wapenzi wa filamu bila shaka tutakuwa tunazungumza lugha moja lakini pia hata kama wewe sio mpenzi wa filamu usiwe na mashaka leo nitakueleza hapa katika Kona ya Filamu.
Leo tunaangukia upande wa Bollywood ambapo tunaangazia filamu ya kusisimua,kusikitisha pamoja na mafunzo ndani yake ikitupa fikra za kutaka kujua ukweli ndani ya gharama za uhuru na kuufikia.
Filamu The White Tiger ilitoka mwaka 2021 kutokana na riwaya yenye jina sawa ya Aravind Adiga ya mwaka 2008.Filamu hii inasimulia maisha ya Balram Halwai, kijana maskini katika kijiji cha India ambaye anapambana kutoka maisha ya umaskini na utumwa hadi kuwa mjasiriamali tajiri.
Balram aliitwa “White Tiger” kwa sababu jina hilo kama kiwakilishi adimu na cha kipekee. Katika filamu White Tiger anatajwa kama mnyama anayepatikana mara moja tu kwa kila kizazi, na ni alama ya upekee, nguvu, na uthubutu.
Jina hilo alipewa na mwalimu wake akiwa shule kwa sababu alionekana kuwa na akili pamoja na uwezo wake mkubwa wa kujifunza ikilinganishwa na watoto wengine katika kijiji alichokua akiishi.
Wahusika katika filamu hii ni Rajkummar Rao na Priyanka Chopra Jonas waliutumia uhusika vizuri kwa kuonesha hali halisi ya mfumo uonevu katika tabaka la chini la wanyonge.
Katika Filamu hii inaangazia ukosefu wa usawa wa kijamii, ubaguzi wa kitabaka, na uharibifu wa mfumo wa kiuchumi na kijamii uliopo nchini kwao India.
Balram akionekana mwenye shauku kubwa na tamaa ya kujikomboa kutoka katika maisha duni aliyozaliwa nayo anapata kazi kama dereva wa familia tajiri na wanasiasa pia anafikiri kuwa kupitia familia hiyo ataweza kuepukana na umaskini.
Wakati akihudumia familia hiyo, anakumbana na unafiki, dhuluma, na ukosefu wa utu unaoambatana na maisha ya shida sana mpaka kusababisha kuchukua hatua kali na kugeuza hadithi ya maisha yake.
Huko Delhi, kwenye siku ya kuzaliwa ya Pinky (Priyanka Chopra), yeye pamoja na Ashok ambaye ni mtoto wa tajiri wakiwa wakiwa wamelewa Pinky anaendesha gari jambo ambalo linamsababishia kugonga na kumuua mtoto kwa isivyo bahati.
Familia ya Stork inamlazimisha Balram kutia sahihi ya kukubali kuwa ni yeye amesababisha ajali hiyo,hali inayomfanya kuogopa baada ya mwajiri wake kumuangushia kesi.
Pinky anaamua kuondoka kwenye familia hiyo baada ya kuona kijakazi kutotendewa haki ndipo Balram anatambua kwamba utumishi mwaminifu kwa Ashok haukuwa hakikisho la maisha yake kwani huduma zake hazihitajiki tena.
Balram anaanza kumlaghai Ashok kwa ankara za uongo, huku akitengeneza pesa pembeni kwa kuuza petroli ya gari la bosi wake na kutumia gari kama teksi kwa siri.
Baada ya maisha kuendelea kua magumu nyumbani kwao ndugu zake wanamtuma mdogo wake aende kujifunza kazi ya udereva na ndipo Balram anamuuwa Ashok na kukimbia na pesa alizokua akitumwa kupeleka rushwa upande mwengine wa serikali.
Cha ajabu alichokifanya Balram ni kutumia zile pesa kuendesha biashara ya teksi na kuajiri vijana wengi waliokosa ajira na wale tabaka la chini ili kuweza kusaidia familia zao.
Filamu hii inatoa fikra kuhusu safari ya kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya mfumo wa kitabaka usio na haki. Pia inatoa mwanga juu ya tamaa ya mafanikio na athari za mfumo wa kijamii unaoweka vizuizi kwa watu wa tabaka la chini.
Kupitia macho ya Balram, filamu hii inakufanya utathmini tena maana ya uhuru na gharama ya kuufikia, pia ikitoa ujumbe mzito kwamba wakati mwingine, ili kufanikiwa ni lazima kuvunja minyororo inayokufunga.




