
KIJANA Madhav Jha kutoka kijijini Patna ana uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa kikapu, lakini hawezi kuzungumza Kiingereza fasaha.
Madhav anajiunga na Chuo cha St. Stephen jijini Delhi, na kujikuta akikubalika sana katika chuo hicho kulingana na kiwango chake cha michezo. Hapo chuoni anakutana na mwanadada Riya Somani, msichana wa kisasa kutoka katika familia ya kitajiri.
Madhav anamsaidia Riya kwa kumfundisha na kushinda mtihani wake unaompa nafasi ya kubakia chuoni. Kisha wanakuwa marafiki wakubwa na wanacheza mpira wa kikapu kila jioni katika uwanja wa chuo.
Madhav anatokea kumpenda sana Riya na siku moja anahudhuria sherehe ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Riya na kumuuliza kuhusu hali ya uhusiano wao.
Riya anamwambia kuwa hawezi kuwa mpenzi wake lakini anaweza kuwa rafiki mpenzi (half girlfriend) yaani kuwa zaidi ya rafiki wa kawaida, lakini si mpenzi.
Madhav, kwa kusumbuliwa na rafiki zake ambao hawaachi kumdhihaki kuwa Riya anataka kumtumia tu na kisha amwache kwenye mataa. Wanamwambia kwamba anapaswa kumshawishi Riya wafanye ngono.
Madhav bila kufikiri anamwomba Riya kumtembelea chumbani kwake kisha anamlazimisha wafanye ngono. Riya anachukia sana na kukimbia, hata hivyo, anakabiliwa na marafiki wa
Madhav ambao wanamcheka na kumdhihaki.
Riya anaamua kumkwepa Madhav na hawakutani tena kwa muda mrefu. Baadaye Madhah
anamfuata Riya na kuomba msamaha lakini Riya bado ana hasira.
Wakati wa sherehe ya chuo, Madhav anaomba tena msamaha, hata hivyo, Riya haoneshi kujali na anampa kadi ya harusi inayoonesha kuwa anaolewa na Rohan, rafiki wa familia yao.
Madhav anaumia sana na anarudi kijijini Patna kumsaidia mama yake anayemiliki shule. Miaka michache baadaye, wakati akimsaidia mama yake shuleni, Madhav anagundua kuwa shule yao inashindwa kuandikisha wanafunzi wa kike kutokana na ukosefu wa vifaa vya chooni.
Serikali ya mtaa haiwezi kuwasaidia kifedha, na hivyo wanaamua kumkabili Bill Gates, ambaye anaitembelea nchi ya India. Anapotembelea Hoteli ya Chanakya kukutana na
ujumbe wa Umoja wa Mataifa, Madhav anagundua kwamba Riya yuko kijijini Patna.
Anamfuata na kugundua kuwa huyu si Riya aliyemfahamu. Ni Riya mpya ambaye amebadilika na ameachana na Rohan na sasa yupo hapo kijijini Patna kwa usaili wa kazi.
Madhav anamwambia Riya kuwa Bill Gates yuko kijijini Patna kuitembelea shule yake na anahitaji kuandaa hotuba ya kumkaribisha. Riya anamwandikia hotuba na Madhav anaweza
kutoa hotuba nzuri sana ingawa Kiingereza kinampiga chenga.
Baadaye Madhav anagundua kuwa Riya kaondoka. Anapata barua kutoka kwa wanafunzi wake iliyoandikwa na Riya kwamba ana kansa ya mapafu na hataweza kuishi muda mrefu.
Madhav analia sana na kuanza kumtafuta Riya kila mahali bila mafanikio.
Miaka michache baadaye, anakutana na Chetan Bhagat anayemwonesha jarida
lililoandikwa na Riya. Madhav anakumbuka kuwa mara nyingi Riya alikuwa akimwambia kuwa alipenda kuwa mwimbaji katika klabu za jijini New York.
Pasipo kutegemea, Madhav anapewa viza ya kuishi jijini New York kwa miezi mitatu tu, na hivyo anapaswa kuhakikisha anampata Riya ndani ya miezi mitatu. Anakwenda jijini New
York kumtembelea rafiki yake Shailesh.
Huko anaanza kumtafuta Riya, bila mafanikio. Shailesh anamuuliza Madhav kuhusu Riya, na anakumbuka tukio la kukutana naye huko Chanakya Hotel. Shailesh anajaribu
kumghilibu Madhav kwa kumkutanisha na mwanadada Anshika, hata hivyo, Madhav haoneshi kumhitaji Anshika.
Ushiriki wa Madhav katika Umoja wa Mataifa unamalizika na marafiki zake wanamfanyia sherehe ya kumuaga. Wakati akiwa ameketi baa, anasikia wimbo ambao amewahi kuusikia
ukiimbwa na Riya.
Kisha anagundua kuwa mwimbaji wa wimbo huo ni Riya mwenyewe. Anamfuata na kugundua kuwa Riya alidanganya kuhusu ugonjwa wake ili aweze kuwa mbali na
Madhav kwa kuwa hakutaka kuwa mzigo kwa Madhav na mama yake.
Filamu ya ‘Half Girlfriend’ ina dakika 130 na imetoka rasmi Mei 19, 2017. Ni moja ya filamu zilizokumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wakosoaji wa filamu nchini India, wakosoaji
wengi nchini humo hawaikubali kabisa.
Hata hivyo, pamoja na ukosoaji mkubwa kwa filamu hii bado hakuna aliyeweza kuwazuia mashabiki na wapenzi wa filamu nchini humo kuigombea kama njugu.
Pamoja na kwamba wakosoaji hao waliegemea zaidi katika kuiponda tu lakini jambo hilo halikuzuia kuifanya filamu hii kushika nafasi ya tisa kwenye filamu 10 bora za mwaka 2017 huku ikifanikiwa kuingiza zaidi ya Dola milioni 14 za Marekani kwenye maonesho ya sinema (box office)pekee.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com




