EPL
Mac Allister aanika ya moyoni kuhusu Liverpool

LIVERPOOL:KIUNGO wa Liverpool, Alexis Mac Allister, amekiri wazi kuwa matumaini ya timu yake kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England yanaonekana kuyeyuka, akisema kwa sasa haoni kabisa dalili za Liverpool kurejea kileleni msimu huu.
Akizungumza kwa huzuni, Mac Allister amesema ni vigumu kukubali lakini uhalisia unaonesha wazi kuwa nafasi ya Liverpool kubeba tena taji ni ndogo sana. Amesema Arsenal wako kwenye kiwango bora, Manchester City wapo karibu, lakini Liverpool wako mbali kimchezo na matokeo. Kwa maneno yake, “Haionekani kama tutakuwa mabingwa tena. Inauma kusema, lakini ukweli uko wazi.”
Nyota huyo raia wa Argentina ameongeza kuwa kinachomuuma zaidi ni kwamba huu ulipaswa kuwa msimu wa kufurahia taji walilolichukua, lakini badala yake wanajikuta kwenye hali ngumu. “Inaniuma, kwa sababu tulipaswa kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kuliko hii tuliyonayo sasa,” amesema.
Mac Allister pia amekiri kuwa mabadiliko makubwa ndani ya kikosi yameathiri mwenendo wa timu. Wachezaji wapya waliingia kuchukua nafasi ya waliotoka, mfumo ukabadilika, na mambo mengi yakageuka kwa wakati mmoja. “Mambo mengi yamebadilika tangu msimu uliopita, na hali siyo nzuri kama tulivyotarajia,” alisema, huku akimalizia kwa kusema yapo mambo mengine anapendelea kubaki nayo moyoni.
Kauli hiyo imewaacha mashabiki wengi wa Liverpool wakiwa na huzuni, ikionesha wazi kuwa hata ndani ya kikosi, imani ya kutetea ubingwa inaanza kupotea.




