Kikapu

TBF yatangaza wachezaji 12 Kanda ya Tano

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limetangaza kikosi cha wachezaji 12 watakaoshiriki michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 16 Kanda ya Tano Afrika, inayotarajiwa kuanza kesho hadi Juni 14, 2025.

Kwa mujibu wa Msemaji wa TBF Mary Arthur, michuano hiyo itafanyika kwenye viwanja vya Filbert Bayi Kibaha, mkoani Pwani. Nchi nyingine zitakazoshiriki ni Uganda, Rwanda na Kenya.

Kikosi hicho chenye wachezaji vijana kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, kinajumuisha majina ya wachezaji wenye vipaji vikubwa ambao tayari wameonesha uwezo mkubwa kwenye michezo ya vijana.

Wachezaji hao ni Richard Ngwira, Praymon Zishi, Calvin Mushi, Raphael Michael, Ibrahim Ramadhani, Brian Munuo, Sarif Benson, Silla Saligwa, Kweli Kweka, John Mgewa, Buchanagandi Ntinika, na Faraji Kayungilo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ismail Mbise, atakuwa akiiongoza kwa kusaidiana na Daudi Maiga na Anasi Kassimu kama makocha wasaidizi.

Arthur alisisitiza kuwa michuano hii ni muhimu kwa kukuza michezo ya vijana nchini na kutoa jukwaa la vijana kuonesha vipaji vyao.

“Michuano ya Kanda ya Tano ni fursa muhimu kwa vijana wetu kuonesha uwezo wao na kupigania nafasi katika timu za taifa za baadaye.,”amesema.

Related Articles

Back to top button