Filamu

ZIFF 2025 kuzinduliwa kesho Zanzibar

ZANZIBAR: TAMASHA la 28 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) linatarajiwa kuzinduliwa kesho Juni 25 hadi 29, 2025 katika viwanja vya Ngome Kongwe visiwani Zanzibar.

Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale amesema tamasha hilo litaanza kwa maandamano ya ufunguzi kutoka kisonge hadi viwanja vya Ngome Kongwe kisha shindano la Mbio za Ngalawa litafanyika. Uoneshwaji wa filamu katika kumbi mbalimbali pia utafanyika na mwisho kutakuwa na usiku wa tuzo ambao utafanyika siku Juni 29 kisha itatangazwa tarehe mpya ya tamasha hilo kwa mwakani.

Naye Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF, Hatibu Madudu amesema wamepokea jumla ya filamu 430 ambapo filamu 174 zinatoka nchi za Afrika Mshariki na nyingine zimetoka nchi nyingine nje ya Afrika Mashariki.

Amezitaja baadhi ya nchi zilizowasilisha filamu zao kwa ajili ya kushindanisha katika tamasha hilo ni pamoja na filamu 49 kutoka Tanzania, filamu 54 kutoka Kenya, filamu 52 kutoka Uganda, filamu 6 kutoka Rwanda, filamu moja kutoka Burundi, filamu 4 kutoka Congo DRC na filamu 8 kutoka Somalia.

Filamu nyingine ni kutoka Irani ambapo wamewasilisha filamu 79, wakati Afrika Kusini wamewasilisha filamu 20 na filamu 36 zinatoka Misri. Filamu nyingine zimepokelewa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo India, Brazil, Marekani, China, Italy, Uturuki, Nigeria, Argentina, Canada, Spain, Ureno, Zimbambwe, Arabuni, Ethiopia, Morocco, Burkinafaso, Ghana na Senegar.

Filamu kutoka nchini Uganda, ‘The Last Stand’ iliyoongozwa na Matt Bish ndiyo itakayofungua pazia la maonesho ya filamu Juni 25 mwaka huu wa 2025 wakati Tamasha la 28 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) litakapozinduliwa kwa msimu mpya kuoneshwa hadi Juni 29, 2025.

Filamu hiyo itakayooneshwa Ngome Kongwe huko Mji Mkongwe viziwani Zanzibar inayoelezea mambo yaliyomtokea kiongozi mmoja wa dini nchini Uganda wakati wa utawala wa Iddi Amin Dada ambapo kiongozi huyo alipambana na bila kuogopa vitisho vya kiongozi wa zamani wa Uganda Idd Amini.

Filamu hiyo imeeleza mambo mengi ambayo hayajulikani lakini yalitokea kwa Kiongozi huyo wa dini na Nduli Iddi Amini licha ya familia ya kiongozi huyo wa dini kumtaka kutompinga rais wa Uganda kwa kipindi hicho lakini yeye alibaki na msimamo wake wa kukemea mabaya yote aliyotenda Idd Amini.

Maduhu amesema katika filamu walizopokea zipo ambazo hazitashindanishwa na nyingine katika tuzo licha ya kuoneshwa katika kumbi za tamasha hilo lakini vigezo vyake havijakidhi kwa ajili ya kushindanishwa hivyo wamezipa heshima ya kuoneshwa ili waweze kujifunza zaidia kwa lengo la kuboresha filamu zao zijazo.

Related Articles

Back to top button