Africa

Yanga yatua Algeria kuwafuata JS Kabylie

ALGIERS: KIKOSI cha Yanga kimewasili Algeria tayari kwa mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie, utakaochezwa Ijumaa wiki hii.

Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amesema dhamira iko kwenye kuhakikisha wanapata ushindi katika uwanja wa ugenini licha ya mchezo kutarajiwa kuwa mgumu na wenye presha kubwa.

“Tunaenda katika mchezo mwingine mgumu dhidi ya JS Kabylie, dhamira yetu ni kupambana na kushinda. Presha lazima iwepo kwa sababu wao wametoka kupoteza mchezo dhidi ya Al Ahly mabao 4-1, watakuja kwa nguvu ili kushinda na sisi tunataka matokeo mazuri, lazima presha iwepo,” alisema Kamwe.

Ameongeza kuwa malengo ya Yanga kwenye mchezo huo ni kuweka rekodi ya ushindi mwingine ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo.

“Malengo yetu ni kushinda mchezo na tutajivunia zaidi kama tutafanya vizuri na kufika hatua za juu,” alisisitiza.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali ya juu baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza dhidi ya AS FAR Rabat bao 1-0 na kujikusanyia pointi tatu, hali iliyoiweka nafasi ya pili kwenye kundi.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, huku Wananchi wakipania kuendeleza rekodi nzuri ya mechi zake zote.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button