Nyumbani

Yanga yabaki Njia Panda Kusubiri Uthibitisho

DAR ES SALAAM:KLABU ya Yanga ipo njia panda kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons baada ya hadi sasa kutosafiri kuelekea mkoani Tabora ambako mechi hiyo imepangwa kuchezwa.

Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, lakini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilitangaza kuufungia uwanja huo juzi kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.

Baada ya uamuzi huo, Tanzania Prisons waliuchagua Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora kuwa uwanja mbadala wa kuutumia kwa ajili ya mchezo huo.

Hata hivyo, Yanga bado haijasafiri kuelekea Tabora huku ikielezwa kuwa klabu hiyo inasubiri uthibitisho rasmi kutoka Bodi ya Ligi Kuu kuhusu mabadiliko hayo.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Rodgers Gumbo, amesema kwa sasa timu hiyo inaendelea na maandalizi yake jijini Dar es Salaam huku wakisubiri mawasiliano rasmi kutoka bodi ya ligi.

“Mpaka sasa bado tunasubiri uthibitisho kutoka Bodi ya Ligi Kuu kuhusu uwanja wa Tabora. Ndiyo maana timu inaendelea na maandalizi hapa Dar es Salaam,” amesema Gumbo.

Mchezo huo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuchezwa kesho kutwa. Yanga wamebanwa na ratiba ngumu kwani baada ya mchezo huo wanapaswa kurudi Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC utakaochezwa Machi 15, mwaka huu.

Related Articles

Back to top button