Ligi KuuNyumbani

Yanga, Simba vitani leo

VIGOGO wa soka nchini, Yanga na Simba wanashuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu katika mechi zao za pili za Ligi Kuu Tanzania Bara leo.

Mabingwa watetezi Yanga, wenyewe watakuwa wa kwanza kucheza wakati watakapokaribishwa na Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia saa 10:00 jioni.

Wakati washindi wa pili wa ligi hiyo msimu uliopita, Simba ambao kabla ya mchezo wa leo wanaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, wenyewe watashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.

Yanga ambayo imechukua mataji yote matatu kutoka kwa Simba, wenyewe wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu sawa na Simba, Mbeya City na Azam, wako katika nafasi hiyo baada ya kushinda 2-1 katika mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania.

Simba walishinda 3-0 dhidi ya Geita Gold, Mbeya City alimaliza kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na Azam FC ilishinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasridene Nabi alisema timu yake itamkosa Djigui Diarra ambaye ni majeruhi wakati wengine ambao hawatacheza leo ni Yacouba Songne, Lazarous Kambole na Salum Abubakari (Sure Boy).

Alisema kikosi chake kinaendelea kukaa vizuri baada ya mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania Union kwenye uwanja huo. Naye kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema maandalizi yamekamilika na wana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya Yanga.

Kwa upande wa Simba, mchezo huo unatarajia kuwa mgumu kwani vigogo hao wanasaka kulipa kisasi baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na baadae Simba kushinda 3-0 katika mchezo wa marudiano. Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola ameeleza kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yako vizuri na lengo lao ni kuondoka na pointi tatu muhimu.

“Ni mchezo mgumu tunawaheshimu Kagera Sugar kutokana na rekodi zao, lakini kwa kutumia ubora wa kikosi chetu naamini tutashinda,” alisema Matola.

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema wamejiandaa vizuri kucheza na Simba ingawa anaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na ukubwa wa wapinzani wao. Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 12 :15 jioni.

Related Articles

Back to top button