Yanga, JKU kupimana ubavu leo

YANGA leo inatarajiwa kupimana ubavu na timu ya JKU kutoka Zanzibar katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, kocha mkuu Nasreddine Nabi alitaka mchezo wa kujipima na timu ya Ligi Kuu kutokana na utaratibu wao hawawezi kucheza na timu ambazo hawajacheza nazo hivyo, waliamua kwenda Ligi Kuu Zanzibar.
Alisema kocha anaamini JKU ni moja ya timu nzuri zitakazowapa ushindani na kujua upungufu wao ili kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC.
“Timu tulizocheza nazo Ligi Kuu ni Kagera Sugar na Geita. Ni ngumu kucheza nazo mechi za kirafiki, ndio maana tulienda Zanzibar. Kocha ameona itakuwa kipimo kizuri cha kujipima kabla ya kwenda kuwavaa KMC katika mchezo ujao wa ligi,” alisema.
Bumbuli alisema programu ya mwezi huu ilikuwa ni kucheza michezo mitatu ya kirafiki na mpaka sasa wamecheza miwili dhidi ya timu ya First League ya Friends Rangers walioshinda bao 1-0 na mwingine unaotarajiwa kuchezwa leo.
Kwa sasa ligi imesimama kupisha timu za Taifa kucheza michezo ya kufuzu Kombe la Dunia na baadhi ya wachezaji wamekwenda kutumikia mataifa yao.
Baadhi ya wachezaji ambao hawakuitwa katika timu za taifa lakini walikwenda kwao kutokana na sababu nyingine ni Jesus Moloko na Djuma Shaban wanaotarajiwa kuwasilia leo wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Bumbuli alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh 5,000 kwa VIP na Sh 3,000 kwa viti vya mzunguko.
Baada ya mchezo huo Yanga inatarajiwa kujiandaa dhidi ya KMC katika mchezo utakaochezwa Oktoba 19, kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.
Yanga imecheza michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Kagera Sugar walioshinda bao 1-0 na dhidi ya Geita walioshinda bao 1-0.