Habari Mpya
Yanga inamalizia, Geita ikitaka kupindua meza

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga na Geita Gold zinashuka madimba tofauti jijini Dar es Salaam leo katika michezo ya marudiano ya michuano hiyo.
Yanga itacheza dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa wakati Geita Gold itapambana na Hilal Alsahil ya Sudan kwenye uwanja wa Azam Complex.
Yanga ina nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao 4-0 Septemba 10 kwenye uwanja huo huo wa Benjamin Mkapa.
Nao Geita Gold leo wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Hilal Alsahil huko Sudan.