Wikiendi ya shangwe na majanga kwa Chelsea

LONDON: WENYEJI wa Darajani Chelsea wamepokea habari mseto kabla ya kuvaana na Everton kwenye Premier League Jumamosi, baada ya kocha Enzo Maresca kuthibitisha kuwa mshambuliaji Cole Palmer na beki wa kati Wesley Fofana wako tayari kurejea uwanjani, huku mshambuliaji Liam Delap akikabiliwa na hadi wiki nne nje kwa majeraha.
Palmer, aliyerejea hivi karibuni kutoka kwenye mapumziko ya wiki sita kutokana na majeraha ya nyonga na kidole cha mguu kilichovunjika, aliachwa kwenye safari ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atalanta ili aendelee kuimarika.
“(Palmer) yuko sawa, yuko vizuri. Kwa sasa anapatikana, jana alimaliza mazoezi akiwa na hisia mchanganyiko, lakini kwa ujumla yuko fiti,” – Maresca amesema.

Beki wa kati Wesley Fofana pia ameruhusiwa kurejea uwanjani baada ya kuondolewa katika mchezo dhidi ya Atalanta kutokana na jeraha la jicho.
“Wesley yuko vizuri. Alikamilisha mazoezi jana,” Maresca aliongeza.
Hata hivyo, Delap hatakuwepo katika mchezo huo baada ya kuumia bega katika sare tasa dhidi ya Bournemouth wiki iliyopita huku kocha huyo akieleza kuwa inaweza kuchukua wiki mbili, tatu au nne kwa mshambuliaji huyo kupona.
Chelsea, ambayo haijashinda katika mechi nne mfululizo, inatafuta kurejesha kasi yao ya mapema msimu ambapo walishinda mechi tisa kati ya 11 kwenye mashindano yote kati ya Septemba na Novemba, ikiwemo ushindi wa 3-0 dhidi ya Barcelona.




