Ligi ya Mpira wa Wavu Dar yazidi kushika kasi

DAR ES SALAAM:LIGI ya Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA) inaendelea kushika kasi, huku timu mbalimbali zikiendeleza ushindani mkali katika mechi zinazoendelea kupigwa kwenye Uwanja wa Kampala, Dar es Salaam.
Michuano hiyo imeingia katika hatua ya lala salama ya kuwania nafasi za kufuzu robo fainali kwa madaraja ya Seria A na B, ambazo zinatarajiwa kuchezwa Juni 1, mwaka huu, katika uwanja huo huo.
Katika matokeo ya mwishoni mwa wiki kwa upande wa wanaume, timu ya KIUT iliibuka na ushindi wa seti 3-2 dhidi ya Bandari, huku Jeshi Stars ikijikuta ikifungwa kwa seti 3-2 na High Voltage. Matokeo mengine yalishuhudia Best Six ikiichapa TCTA kwa seti 3-0, TPDC ikiilaza Giraffe kwa seti 3-0, na IP Sports ikiibuka na ushindi wa seti 3-1 dhidi ya UDSM. Twalipo ilikubali kichapo cha seti 3-0 kutoka kwa Kigamboni, na Nyika ikaitandika Wazo kwa seti 3-0.
Kwa upande wa wanawake, KIUT iliichapa Tanzania Prisons kwa seti 3-2, huku Chui ikisajili ushindi wa seti 3-0 dhidi ya TPDC na pia ikapata ushindi wa mezani dhidi ya UDSM. Timu ya Wazo ililazwa kwa seti 3-0 na Tai.
Akizungumza na SpotiLeo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ya Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA), Peter Kahwaa, amesema kuwa maendeleo ya ligi hiyo ni mazuri na timu zimeendelea kuonesha ushindani wa hali ya juu katika harakati za kufuzu hatua ya robo fainali.
“Nawaomba mashabiki na wapenzi wa mpira wa wavu wajitokeze kwa wingi kushuhudia vipaji na burudani kutoka kwa wachezaji wetu kila Jumamosi na Jumapili hapa Uwanja wa Kampala. Kiingilio ni bure kabisa,” amesema Kahwaa.
Amewaomba wadau na wafadhili kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kusaidia kufanikisha ligi hiyo pamoja na kuiwezesha jumuiya ya timu shiriki