Burudani

Wasanii wa filamu wakemea kauli za viongozi wa zinazohatarisha amani

DAR ES SALAAM:BAADHI ya wasanii wa filamu nchini wamejitokeza kukemea vikali kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambazo zinaashiria uchochezi na uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari, msanii Jimmy Mafufu alisema ni muhimu kwa viongozi wote wa kisiasa kuwa na tahadhari katika matamshi yao ili kulinda amani ya nchi.

“Ni wakati sasa wa kukemea uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa. Kauli zinazohamasisha vurugu haziwezi kufumbiwa macho. Amani ikipotea, haipatikani kwa urahisi,” amesema Mafufu.

Aidha, aliwataka viongozi wa dini kutotumia nyumba za ibada kama majukwaa ya kuhamasisha vurugu au kutoa matamshi yanayochochea migawanyiko.

Akizungumzia matamshi yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa chama cha Chadema, Mafufu amesema: “Kauli za kusema kitanuka si za kujenga bali ni za kuvuruga amani. Chadema kwa sasa hakina jipya, chama chao kimeshapoteza mwelekeo na wanahitaji kuanza upya — na kuanza upya si ujinga.”

Kwa upande wake, msanii mwingine, Chick Mchoma, alisisitiza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa na lugha ya kutuliza na si kuchochea.

“Tanzania iko shwari. Hatudanganyiki. Tuko tayari kupiga kura. Kauli za kuvuruga Katiba au amani ya nchi hatutazikubali. Sisi kama vijana hatutakaa kimya. Tutapinga kwa nguvu zote,” amesema Mchoma.

Wasanii hao pia walieleza kuwa vijana wengi wako tayari kushiriki uchaguzi mkuu ujao na wanatambua juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Related Articles

Back to top button