Muziki

Waimbaji wa injili, viongozi wa dini watakiwa kuliombea taifa

DAR ES SALAAM:KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Emmanuel Nchimbi, amewataka waimbaji wa nyimbo za Injili pamoja na viongozi wa dini nchini kutokata tamaa katika kulitumikia Taifa kwa maombi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwaombea viongozi wa nchi ili kuendelea kudumisha amani, furaha na mshikamano.

Akizungumza katika tamasha la Mtoko wa Pasaka lililoandaliwa na mwimbaji wa Injili Christina Shusho kwa kushirikiana na Mama Ongea na Mwanao, Balozi Nchimbi alisema maombi ni silaha muhimu na yanapaswa kuwa endelevu.

“Msichoke kuliombea Taifa, kuwaombea viongozi wetu ili tuendelee kuwa na nchi ya amani na furaha. Msiache pia kuwakumbusha wanasiasa, maana mara nyingine tunapokuwa kwenye vipaza sauti tunajisahau. Tukikaa pembeni tunajiuliza, ‘Je, ni mimi niliyesema haya yote?’,” alisema Nchimbi.

Alisisitiza kuwa si vibaya kiongozi kukiri makosa pale anapoteleza kwa kauli, kwani kusema “samahani” hakumpunguzii chochote.

“Usione aibu kusema ‘jamani hapa nimekosea, ulimi umeteleza’. Kauli ya kiongozi mmoja inaweza kubadilisha hali ya Taifa. Hivyo ni muhimu kuwa makini na maneno yetu,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Balozi Nchimbi aliwapongeza wasanii wa Injili kwa kazi kubwa wanayoifanya kusaidia jamii, hususan wagonjwa, yatima, wajane na wagane. Alisema matendo hayo ni ya kuigwa na yanapaswa kuendelezwa.

“Ni jambo la kufurahisha kuona jinsi ambavyo mnajitoa kuwafariji wenye uhitaji. Kila Mtanzania anapaswa kutambua thamani ya kuwajali wengine, hususan wale waliopo katika mazingira magumu,” alisema.

Steve Nyerere na Christina Shusho walikabithi zawadi picha inayowaonesha Rais Samia Suluhu na Balozi Nchimbi ikiwa imebeba ujumbe wa Mtashinda.

Related Articles

Back to top button