KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema ushindani Ligi Kuu Tanzania Bara umekuwa mkubwa hivi sasa hivyo wachezaji wa timu hiyo hawapaswi kufanya mzaha hata kidogo.

Akizungumza na SpotiLeo, kocha huyo amewataka wachezaji wa timu hiyo kuacha kuliwazia suala la kiungo Feisal Salum badala yake wafikirie zaidi umuhimu wa kushinda mechi zinazowakabili.
Amesema Feisal ni muhimu kwenye timu lakini wanapaswa kuwaachia viongozi na wao kuelekeza nguvu zao kwenye mbio za ubingwa.
“Jukumu letu ni kuhakikisha Yanga inaendelea kupata ushindi katika kila mechi iliyopo mbele yetu hilo ndio la msingi kwa sasa,” amesema Kaze.
Yanga inaongoza msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 47 huku watani wao Simba ikiwa na pointi 41 katika nafasi ya pili wakati Azam ipo nafasi ya tatu ikikusanya pointi 37 na timu zote tatu zinalingana idadi ya michezo 18.




