Michezo Mingine

Wachezaji 500 wa vishale (Darts) kuchuana Arusha

DAR ES SALAAM:WACHEZAJI 500 kutoka nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kukutana katika michuano miwili ya wazi ngazi ya klabu na taifa itakayofanyika kuanzia Juni 27, mwaka huu mkoani Arusha.
 
Akizungumza na SpotiLeo, Katibu Mkuu wa Chama cha Darts (Vishale) Tanzania (TADA), Innocent Joseph, amesema hayo ni mashindano makubwa ya kwanza kufanyika chini ya uongozi wao mpya mwaka huu, yakitarajiwa kufanyika kwenye Bwalo la Magereza mkoani humo na kushirikisha idadi kubwa ya wachezaji.
 
Amesema mashindano hayo yataanza na ngazi ya klabu, ambapo wachezaji kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Kagera, Kilimanjaro, Dodoma na mingine watashiriki kupitia vilabu vyao.
 
“Tutaanza na ngazi za klabu tukitegemea kuangalia viwango vya wachezaji wetu. Hapa kutakuwa na wachezaji mmoja mmoja, wawili, na kama timu. Siku ya mwisho tutamalizia na mashindano yatakayohusisha timu za taifa,” amesema Joseph.
 
Kwa mujibu wa Joseph, michuano ya pili itawakutanisha wachezaji wa timu za taifa kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
 
Amesema maandalizi yanaendelea vizuri na timu zote zinajipanga ili kushiriki kwa ushindani na kutafuta ushindi.
 
Joseph pia ameomba wadau, taasisi na kampuni mbalimbali kuwaunga mkono kuelekea mashindano hayo, kwa kusaidia kutoa motisha kwa wachezaji na kuwezesha kufikiwa kwa malengo waliyojiwekea.
 

Related Articles

Back to top button