Waamuzi Dabi ya Kariakoo vilio

DAR ES SALAAM: MWAMUZI Msaidizi namba moja (1) wa mchezo dabi ya Simba na Yanga, Kassim Mpanga kutoka Dar es Salaam, amefungiwa miezi sita (6) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu ambapo katika dakika ya 70 ya mchezo alikataa bao halali la klabu ya Simba kwa kile alichoonesha kwamba kulikuwa na kosa la kuotea kabla ya kufungwa kwa bao hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi iliyotolewa leo, taarifa ya wataalam wa kutafsiri sheria za mpira wa miguu, baada ya kufanyia tathmini video ya tukio hilo, imebainisha kwamba hakukuwa na kosa lolote kabla ya kufungwa kwa bao hilo.
Mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo tajwa hapo juu, Hamdan Said kutoka Mtwara amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu ambapo katika dakika ya 61 ya mchezo aliashiria kuwa mchezaji Prince Dube wa klabu ya Yanga alikuwa katika eneo la kuotea, hivyo kusimamisha shambulizi ambalo klabu ya Yanga ilikuwa inafanya langoni mwa Simba.
Hata hivyo, taarifa ya wataalam wa kutafsiri sheria za mpira wa miguu, baada ya kufanyia tathmini video ya tukio hilo, imebainisha kwamba mchezaji huyo hakuwa katika eneo la kuotea wakati mpira huo unapigwa kuelekea kwake.
Mwezi Desemba 2025, mwamuzi huyo aliadhibiwa kwa kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kutokana na makosa ya aina hii.
Katika hatua nyingine, mechi ya Simba na Dodoma Jiji, Mwamuzi wa akiba Charles Simon kutoka Dodoma amefungiwa miezi mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kuruhusu klabu ya Dodoma Jiji kufanya mabadiliko ya wachezaji katika mikupuo minne (4) badala ya mitatu (3) kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:32 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Aidha, Mwamuzi wa kati Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida aliyechezesha mchezo kati ya Namungo na Yanga ameshushwa daraja la uamuzi kwa makosa ya kujirudia ya kushindwa kutafsiri vema sheria.
Pamoja na matukio mengine, mwamuzi huyo alishindwa kutafsiri sheria katika tukio la mchezaji Abdulkarim Kiswanya wa Namungo kuvutwa jezi na mchezaji Mussa Damaro wa Yanga ndani ya eneo la penati, hivyo kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za mpira.



