Kwingineko
Vurugu kuwapeleka Lyon kwenye CCTV

LYON:MABINGWA wa zamani wa Ligue 1 ya Ufaransa klabu ya Olympique Lyon imesema itapitia video za camera za CCTV ili kuwabaini mashabiki walioanzisha vurugu baada ya klabu hiyo kuondoshwa kwenye michuano ya kombe la Ufaransa na klabu ya ligi daraja la 5 nchini humo ya FC Bourgoin-Jallieu kwa mikwaju ya penati usiku wa kuamkia leo.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo mapema leo asubuhi imesema klabu hiyo haivumilii aina yeyote ya uvunjifu wa amani na vurugu mchezoni huku ikiueleza pia umma itaushirikisha uongozi wa klabu hiyo katika maamuzi yatakayofikiwa.
“OL haivumilii aina yoyote ya vurugu kutoka kwa mashabiki wetu, tunafanya mawasiliano na FC Bourgoin-Jallieu na tutapitia picha za CCTV kuwabaini wahusika wa kadhia hii. Iwe ya maneno nguvu au ubaguzi. Matukio kama haya hayataachwa yachafue jina letu.”- imesema taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa X.
Mashabiki wa FC Bourgoin-Jallieu ndio walikuwa wa kwanza kuingia eneo la kuchezea baada ya penati ya mwisho ya Mehdi Moujetzky kuzama nyavuni kisha wale wa Olympique Lyon nao kuingia eneo hilo na kuzuka ugomvi mkubwa
Mikwaju ya penati iliamua mchezo huo baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.