Vijana 295 wajitokeza michuano ya kuogelea

DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya Taifa ya Kuogelea kwa vijana yameweka historia mpya baada ya kuvutia washiriki 295 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na hata Kenya, ikiwa ni mara ya kwanza kwa idadi hiyo kubwa ya wachezaji kushiriki.
Akizungumza katika mashindano hayo yaliyoanza Dar es Salaam Leo, Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania, David Mwasyoge, amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya kalenda rasmi ya chama na yana lengo la kuibua vipaji kuanzia ngazi ya chini.
“Haya ni mashindano ya maendeleo kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi kumi na mbili. Tunawapa jukwaa la kupata uzoefu na maandalizi ya mashindano makubwa ya baadaye,” amesema.
Amesema mashindano haya ndiyo yamehitimisha msimu wa mwaka wa mashindano wa 2025/26, ambapo kwa mara ya kwanza wameweza kufikia idadi kubwa ya washiriki wa ndani ya nchi.
Mwasyoge alieleza kuwa miaka ya nyuma, asilimia kubwa ya washiriki walikuwa kutoka nje ya nchi, lakini safari hii watoto wengi waliokuwa mashindanoni ni Watanzania.
“Miaka kumi au kumi na tano iliyopita, asilimia 90 ya washiriki walikuwa si Watanzania. Lakini leo hii, asilimia 100 ni watoto wa Kitanzania. Hili ni jambo la kujivunia,” ameongeza.
Amesema mafanikio haya yanatokana na muamko mkubwa wa wazazi, klabu na wadau wa michezo, sambamba na ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kukuza mchezo wa kuogelea nchini.