Vigogo wahaha kumbakisha Ronaldo Saudia

RIYADH: CHANZO cha kuaminika kutoka ndani timu ya mzungumzo ya makubaliano kimeliambia Shirika la Habari la AFP kuwa kinafahamu maafisa kutoka nchini Saudi Arabia wapo katika mazungumzo ‘magumu’ ya kumshawishi mshindi mara 5 wa tuzo ya mwanasoka bora wa Dunia Cristiano Ronaldo kusalia nchini humo.
Mazungumzo haya yanakuja baada ya Ronaldo mwenye miaka 40 kuandika ujumbe kupitia mitandao yake ya kijamii kuashiria kuwa anataka kuondoka Al Nassr huku tetesi zikisema gwiji huyo anaweza kutimkia timu yeyote miongoni mwa timu 30 shiriki za kombe la Dunia la Klabu linalotarajia kuanza Katikati mwa mwezi June.
“Kuna mazungumzo ambayo kwakweli ni magumu ya kumshawishi Ronaldo abaki Saudi Pro League msimu ujao. Moja kati ya machaguo ni asajiliwe na Al Hilal wenye tiketi ya michuano ya Kombe la Dunia au ahamie kwa mabingwa wa kombe la Asia Al Ahli lakini tunataka abakie” – kimesema chanzo hicho ambacho ni afisa wa mfuko wa uwekezaji ambao ni wawekezaji wakubwa kwenye ligi kuu.
Rais wa FIFA Gianni Infantino wiki iliyopita alisema “kuna majadiliano” juu ya nyota huyo wa zamani wa United, Real Madrid, Juventus na Sporting Lisbon acheze kwenye michuano hiyo iliyotanuliwa nchini Marekani inayoanza Juni 14.
Dirisha maalum la usajili linafunguliwa kuanzia Juni 1hadi 10 kuruhusu timu 32 zinazoshiriki Kombe la Dunia la Klabu kusajili wachezaji. Mshambuliaji huyo wa Ureno alijiunga na Al Nassr mwaka wa 2022 akitokea Manchester United na mkataba wake unamalizika mwishoni mwa mwezi ujao.




