BurudaniFilamu

UNTRACEABLE

MPELELEZI maalumu wa Shirika la Upelelezi la nchini Marekani (FBI), Jennifer Marsh, anafanya kazi kwenye kitengo maalumu kinachoshughulikia uhalifu wa kimtandao cha shirika hilo la upelelezi la Marekani.

Katika kazi zake anashirikiana na Griffin Dowd kupambana na uhalifu unaofanywa na watu wanaoiba taarifa na utambulisho wa wengine na kuzitumia katika uhalifu.

Jennifer anaishi katika kitongoji kimoja kwenye mji wa Portland na binti yake, Annie Haskins na mama yake, Stella Marsh, baada ya kufiwa na mumewe.

Usiku mmoja, wakiwa katika kufuatilia taarifa za uhalifu wanagundua kuhusu chanzo kimoja kisichojulikana kinachowaongoza kwenye mtandao wa intaneti unaoitwa KillWithMe.com. Mtandao huo unaonesha video ya paka anayeteswa na kisha kuuawa.

Wapelelezi hawa wanajaribu kuufunga mtandao huo lakini wanashindwa kuufunga, kwani mtengenezaji wake alijua tangu mwanzo kwamba kuna mtu angejaribu kuufunga na hivyo akauwekea kinga salama; kila wakati seva inajifunga, na seva mbadala hujitokeza mara moja.

Baada ya kifo cha paka huyo, msimamizi wa mtandao huo wa KillWithMe.com anahamia katika kutesa watu, anawateka nyara na kuwaweka katika chumba
maalumu chenye mitego ya kifo.

Mwathirika wa kwanza wa sakata hilo ni rubani mmoja wa helikopta, ambaye anakufa kwa kutokwa damu nyingi kutokana na kuchomwa sindano za anticoagulant,
dawa inayozuia damu kuganda.

Baada ya mauaji ya rubani yanafuatia mauaji mengine yanayomhusisha mtangazaji
wa habari ambaye anachomwa hadi kufa na taa zenye joto kali sana wakati akiwa
amesakafiwa kwa saruji sakafuni.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa Shirika la Upelelezi la
Marekani anautaka umma kuuepuka mtandao huo wa KillWithMe.com ili wasiingie
katika matatizo, lakini badala yake, kama mpelelezi Jennifer alivyohofia, jambo
hilo linauongezea umaarufu mtandao huo na watu wengi wanaanza kuufuatilia.

Jennifer, Griffin na wapelelezi wengine wanajitahidi kumfuatilia mhalifu anayemiliki mtandao huo lakini inawawia vigumu kwa kuwa anatumia kompyuta za watu wengine alizoziteka nyara kupitia mtandao wa intaneti na kusambaza taarifa zake huku akificha utambulisho wa eneo alilopo.

Jambo wasiloelewa ni kwamba mhalifu huyo yupo hapo hapo Portland. Hili ni jambo la hatari na Jennifer anahofia kuwa anaweza kuwa tishio kwake, kwa binti yake Annie na kwa mama yake.

Mara mpelelezi mwenza wa Shirika la Upelelezi la Marekani, Griffin anatekwa nyara baada ya kuchunguza chanzo kinachomwongoza kwenye utambulisho wa eneo alilopo muuaji na kisha kupokea simu kutoka kwa muuaji anayeficha sauti yake na kujifanya kama mmoja wa
wapenzi wa Griffin.

Katika chumba cha chini kwenye jengo linalotumiwa na muuaji, Griffin anazamishwa kwenye shimo la maji hadi shingoni kwake huku mdomo wake ukiwa umefungwa kwa gundi
maalumu, kisha mtego wa kifo unaingiza ndani ya maji hayo mkusanyiko wa tindikali
ya sulphuric.

Baada ya muuaji kutoka chumbani, Griffin anatumia nyakati zake za mwisho kabla ya kufa kufinya ujumbe maalumu kwenye mfumo wa kipelelezi wa morse, anatoa taarifa kwa uongozi wa Shirika la Upelelezi la Marekani kuhusu suala alilokuwa anafuatilia.

Mpelelezi Jennifer anaufuatilia mfumo huo uliotuma ujumbe wa morse na kugundua kuwa waathirika wote waliwekwa eneo moja; walihusishwa katika urushwaji wa matangazo na kadhalika.

Mtoto wa mwalimu wa chuo anayehusishwa na uhalifu huo, Owen Reilly anavunjika na kulazwa katika hospitali ya magonjwa ya akili. Na anaporuhusiwa, anaamua kulipiza kisasi kwa wale ambao anahisi wamehusika katika kifo cha baba yake.

Polisi wanavamia nyumba ya Owen lakini hawamkuti. Muda wote Owen anamfuatilia Jennifer kwa sababu sasa anamhitaji.

Anamnasa na kumweka kwenye mtego wa kifo kwa muda kwa kumtundika juu na kumshusha polepole hadi kwenye eneo la kifo chake wakati watu wengi wanafungua mtandao huo kujionea.

Jennifer anafanikiwa kutoroka kwa kuning’inia na kurukia kwenye nguzo inayomfikisha hadi chini. Kisha anampiga risasi Owen na kumjeruhi wakati polisi wanafika eneo hilo. Kifo cha Owen kinarushwa kwenye vyombo vya habari kama ilivyokuwa kwa baba yake.

Kisha Jennifer anaonesha beji yake ya FBI kwenye kamera ya mtandao huo. Filamu ya Untraceable ya mwaka 2008 imeongozwa na Gregory Hoblit, ina dakika 101 na imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 35 na imefanikiwa kuingiza dola milioni 52.7.

Filamu hii ilipotoka ilikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wakosoaji wa filamu wa mtandao wa Rotten Tomatoes ambao ameipa alama 16 kati ya 100 kutokana na maoni 149.

Licha ya ukosoaji huo lakini ukweli ni kwamba imetengenezwa kwa umakini na ustadi. Inaonesha aina ya vitu ambavyo kutokujulikana kwa mtandao wa intaneti huvifanya viwezekane.

 

0755 666964 au bhiluka@gmail.com

Related Articles

Back to top button