
DAR ES SALAAM:KAMA ilivyo desturi, Official Baba Levo mara kwa mara humuita msanii Diamond Platnumz kwa jina la Lukuga. Lakini je, umewahi kujiuliza jina hilo limetoka wapi na lina maana gani?
Jina hilo limetokana na Mto Lukuga, mto mkubwa unaopatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mto huu huanzia Ziwa Tanganyika na ni njia pekee ya maji kutoka ziwani humo kuelekea Mto Kongo, kisha hatimaye kuishia katika Bahari ya Atlantiki.
Lakini Lukuga si jina la mto wa kawaida tu. Takriban 18% ya maji yote yanayopotea kutoka Ziwa Tanganyika hupitia mto huu. Hali hii imechangia kupungua kwa kina cha ziwa hilo, jambo lililowalazimu wataalamu kutoka Tanzania, DRC na Burundi kushirikiana katika tafiti mbalimbali za kutafuta suluhisho la kulinda ziwa hilo muhimu.
Moja ya masuluhisho yaliyoibuliwa ni kujengwa kwa uzio maalum katika Mto Lukuga ili kudhibiti kasi ya upotevu wa maji.
Mto Lukuga hubadilika mtiririko wake kulingana na misimu na hali ya hewa; una nguvu ya kupeleka kile kinachokusanywa mbali na huathiri mfumo mkubwa wa ikolojia. Hali hii inafananishwa na jinsi Diamond Platnumz anavyoathiri mfumo mzima wa muziki Afrika Mashariki, ndio maana Baba Levo humuita Lukuga.