Ujumbe wa Kimahaba wa Jay Melody Gumzo

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Sharif Juma ‘Jay Melody’ ameibua mjadala mitandaoni baada ya kuposti picha akiwa na mwanamke ambaye hajafahamika rasmi, huku akiambatanisha na ujumbe wa kimahaba uliozusha maswali mengi kutoka kwa mashabiki wake.
Katika picha hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Jay Melody aliandika:
“Mizigo yako nitajitwika, niko tayari mie kuanza safari.”
Ujumbe huo umeibua hisia mseto miongoni mwa mashabiki, huku baadhi wakiamini huenda msanii huyo ameweka wazi uhusiano wake wa kimapenzi, huku wengine wakihisi ni dondoo ya kazi mpya ya muziki inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.
Jay Melody, anayefahamika kwa sauti yake ya kipekee na nyimbo zenye maudhui ya mapenzi, hajatoa ufafanuzi wowote kuhusu picha hiyo wala maelezo ya mwanamke aliyeonekana naye.
Hata hivyo, historia yake katika tasnia ya muziki imejaa ubunifu wa kutumia hisia katika kutangaza kazi mpya, hali inayopelekea wengi kudhani huenda huu ni mwanzo wa kampeni ya kutambulisha wimbo au video mpya.
Kwa sasa mashabiki wake wanasubiri kwa hamu kuona kama ujumbe huo ni tangazo rasmi la mahusiano mapya au sehemu ya mwelekeo mpya wa kisanii.