Uganda yaibuka kinara, yazoa tuzo 5 za ZIFF 2025

ZANZIBAR: TAMASHA la 28 la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) la mwaka 2025, limehitimishwa huku waigizaji kutoka Uganda wakiibuka na shangwe kubwa visiwani Zanzibar baada ya kunyakua tuzo 5 na kuwazidi washiriki wote katika tuzo hizo.
Katika usiku huo wa tuzo ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Thabiti Kombo, Uganda iliibuka na tuzo ya Filamu Bora (Feature Film) kupitia Filamu ya ‘JANANI THE LAST STAND’ , iliyoongozwa na Matt Bish; kupitia filamu hiyo muigizaji Peter Odeke, amenyakua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kiume (Afrika Mashariki).
Tuzo nyingine waliyoshinda Uganda ni tuzo ya Filamu Fupi (Short Film),kupitia filamu ya ‘Boy No Fear’ iliyoongozwa na Jonathan Curtiss.
Uganda pia imenyakua Tuzo ya dokumentari bora kupitia filamu ya ‘Memories of Love Returned’ kutoka Uganda, iliyoongozwa na Ntare Guma Mbaho Mwine.
Tuzo nyingine ni muigizaji bora wa kike katika tamthilia Afrika Mashariki iliyonyakuliwa na Mirembe Doreen (Damalie) nayo inatoka Uganda.
Pamoja na mafanikio haya makubwa ya Uganda, Kenya imeonesha ubora wake kupitia ‘KILEO’ ya Bill Jones Afwan iliyoshinda Filamu Bora ya Afrika Mashariki, huku Jimmy Gathu ‘Chocolate Empire’ akitwaa tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume katika Tamthilia (Afrika Mashariki), na ‘SUBTERRANEA’ ya Likarion Wainaina ikishinda Tamthilia Bora ya Afrika Mashariki.
Tanzania, kama mwenyeji, pia haikuachwa nyuma. Shamira Ndwangila ‘Kombolela’ amenyakua tuzo ya Muigizaji Bora wa Kike katika Tamthilia (Tanzania), Kojack Chillo ‘Jacob’s Daughters’ akiwa Muigizaji Bora wa Kiume katika Tamthilia (Tanzania), na ‘KOMBOLELA’ ya Mustapha Machupa ikishinda Tamthilia Bora ya Tanzania. Katika Filamu Bora, Wisher Nakamba ‘Niko Sawa’ aliibuka na tuzo mbili Muigizaji Bora wa Kike (Tanzania) na Hemedy Suleiman aliibuka Muigizaji Bora wa Kiume (Tanzania).
Tuzo za ZIFF Chairman’s Award zilienda kwa ‘SHABAKADDA’ kutoka Somalia, ‘THE HOUSE OF RISING HOPE’ kutoka Urusi, na ‘BELIEVE’ kutoka Jamaica nayo imeshinda tuzo hizo.