Tuzo ya goli bora! Mzize awapa tano mashabiki

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Clement Mzize, ametoa shukrani kwa mashabiki na wote waliomuunga mkono baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Goli Bora Afrika, katika hafla ya utoaji wa tuzo za CAF iliyofanyika jana nchini Morocco.
Mzize alishindwa kuhudhuria katika hafla hizo kutokana na majeraha baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.
Kupitia mtandao wake Mzize aliweka video ya shukrani na kuandika ujumbe huu: “Mwenyezi Mungu awabariki sana mashabiki kwa kupiga kura na kufanikisha kutwaa tuzo hii.”
Akaongeza kwa kuwapongeza wachezaji wenzake na benchi la ufundi kwa ushirikiano uliowezesha mafanikio hayo.
Mzize pia, aliwashukuru viongozi wa klabu kwa kusimama na timu katika kila hatua huku akisema kuwa tuzo hiyo ni ya mafanikio ya pamoja.
Wachezaji mbalimbali walimpongeza wakiwemo mchezaji wa Azam FC Feisal Salum, nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto, Aucho Khalid wa Singida Black Stars, Simon Msuva anayecheza soka la kulipwa Iraq na wadau mbalimbali.




