
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema yeye na wachezaji wenzake wameupania mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Simba Oktoba 23 lengo likiwa kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi ya ligi.
Akizungumza na Spotileo, kiungo huyo amesema wanataka kuanza na Simba na baadaye Club African katika mchezo wa mtoano kabla ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda ili kuwafurahisha mashabiki wetu ambao kwa kiasi kikubwa wamechukia kutolewa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Fei Toto.
Yanga itakuwa wenyeji wa Simba uwanja wa Benjamin Mkapa huo ukiwa ni mchezo wa kwanza kati ya timu hizo kwenye ligi msimu huu.
Katika mchezo wa mwisho Yanga na Simba kukutana Ligi Kuu Aprili 30 2022, timu hizo zilitoka suluhu.