Tujitume, tusijivunie rekodi zilizopita-Bocco

BAADA ya Simba kupangwa Kundi C Ligi ya Mabingwa Afrika Nahodha wa miamba hiyo ya soka nchini John Bocco amewataka wachezaji wenzake kucheza kwa kujituma zaidi na siyo kujivunia rekodi zao za mashindano yaliyopita.
Akizungumza na SpotiLeo Bocco amesema kucheza kwa mazoea kunaweza kuwavurugia mipango na kushindwa kufikia malengo>
“Ili tuweze kufikia malengo yetu lazima tucheze mechi hizi za makundi kwa kujitoa na kujituma bila kuangalia kuwa tuna uzoefu kiasi gani,” amesema Bocco.
Nahodha huyo wa Simba amesema kundi hilo gumu na wanapaswa kupambana kuonesha ukumbwa wao katika mashindano hayo.
Wakati huo huo Kocha MKuu wa Simba, Juma Mgunda amesema ugumu wa kundi C unatokana na timu zote zilizopangwa kundi hilo kushiriki mara kwa mara michuano hiyo.
“Tumepangwa kundi C na timu za Horoya AC, Raja CA na Vipers timu zote ni nzuri na tunaziheshimu sababu ukiangalia rekodi zao mpaka zimefika hapo zimezitoa timu kubwa Afrika pengine kuliko sisi,” amesema Mgunda.
Amesema Simba inatarajia kukiongezea nguvu kikosi chake katika dirisha dogo, usajili anaoamini utakuwa na faida kubwa katika hatua hiyo ya makundi.