Tobey Maguire asimamia ndoa ya mtalaka wake

HAWAII: NYOTA wa filamu za Spider-Man, Tobey Maguire amestaajabisha umma baada ya kuongoza shughuli nzima ya kumfungisha ndoa aliyekuwa mkewe, Jennifer Meyer.
Tobey, 51 alikuwa mwongozaji wa tukio la kula kiapo cha ndoa baina ya Jennifer, 49 ambaye ni mbunifu maarufu wa vito na bilionea, Geoff Ogunlesi, 34.
Hafla hiyo ya faragha ilifanyika kwenye hoteli ya kifahari ya Four Seasons Resort na kuhudhuriwa na watu maarufu wa Hollywood; Leonardo DiCaprio na mpenziwe, Vittoria Ceretti, Jeff Bezos, Courteney Cox na Rachel Zoe.
Watoto wawili wa Tobey na Jennifer, Ruby, 19 na Otis, 17, nao walishiriki katika shughuli hiyo.
Aidha Jennifer na Geoff pia walijaaliwa mtoto wao wa kike mwezi Mei, mwaka huu, wakiongeza mtoto mwingine kwenye familia hiyo iliyochanganyika.
Tobey na Jennifer, walioana mwaka 2007 kabla ya kutengana mwaka wa 2016 na Jennifer kuwasilisha kesi ya talaka Oktoba 2020. Na talaka yao ilikamilika rasmi Oktoba Mosi, mwaka huu.
Kwenye mitandao ya kijamii wengi wamemsifu Tobey kwamba licha ya kuachana kimapenzi, lakini wawili hao wameweka ustaarabu na heshima mbele zaidi na kuweka mfano mzuri wa kuachana sio uadui.




