Habari Mpya

Timu za Tanzania mguu sawa michuano ya CAF

WIKI ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imefi ka na Tanzania ipo tayari kuzishuhudia timu zake sita zikipeperusha vyema bendera yake kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya, ikiwemo usajili wa gharama kubwa.

Kutoka Tanzania Bara klabu za Yanga na Simba zitashiriki Ligi ya Mabingwa wakati Azam FC na Geita FC zenyewe zitacheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf).

Kwa upande wa Zanzibar, wenyewe watawakilishwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo au maarufu kama KMKM katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Kipanga FC itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho.

RATIBA KAMILI

Ratiba inaonesha timu tano za Tanzania zitaanza kampeni hiyo zikiwa ugenini timu hizo ni Simba, ambayo itakuwa Blantyre ikicheza na Nyasa Bullets, Geita FC itakuwa Sudan dhidi ya Hilal Al Sahil, Yanga ilipangwa kuanzia ugenini lakini kutokana na usalama kuwa mdogo Sudan Kusin sasa mechi yake dhidi ya Zalan itachezwa uwanja wa Azam Complex, Yanga wakiwa wageni.

Kipanga FC nayo itaanzia ugenini dhidi ya Hilal FC Wau ya Sudan Kusini mchezo ambao umepangwa kupigwa Septemba 11 na Mabingwa wa Zanzibar KMKM ndio timu pekee kutoka Tanzania itakayoanzia nyumbani kucheza na Al Ahli Tripoli ya Libya.

Kwa maandalizi ambayo timu zote zimeyapata hapana shaka mechi hizo za ufunguzi zitaleta matokeo chanya na kufufua matumaini ya kusonga mbele kwenye hatua zinazofuata kwenye mashindano wanayoshiriki.

YANGA

Yanga inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele raundi ya kwanza kutokana na udhaifu wa mpinzani iliyepangiwa naye Zalan FC timu ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo, lakini ubora wake nao unatia mashaka ukilinganisha na wawakilishi hao wa Tanzania.

Kucheza mechi zote mbili kwenye ardhi ya nyumbani nayo inaweza kuwa faida kubwa kwa Yanga, ambayo inalazimika kucheza na kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ili kutengeneza rekodi na heshima na kuogopewa kwenye raundi zinazofuata.

Baada ya kutolewa kwenye hatua ya awali kwenye michuano hiyo msimu uliopita, msimu huu Yanga inaingia kwenye michuano hiyo ikiwa imejipanga kweli kweli kuanzia kwenye usajili na hata maandalizi yao lengo lao likiwa kufika angalau nusu fainali kama siyo kubeba ubingwa.

SIMBA

Simba leo Jumamosi itakuwa Blantyre Malawi kuanza na Nyasa Big Bullets siyo mchezo rahisi kutokana na ubora waliokuwa nao wenyeji wao, lakini rekodi ya Simba katika michuano hiyo inatisha na wenyeji wana kazi ya kufanya na wenyewe wanalijua hilo.

Simba ilishatua Blantyre tangu Alhamisi ikiwa na kikosi kamili na lengo lake kubwa ni kuendeleza rekodi yao nzuri ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo katika miaka ya hivi karibuni imeweka rekodi ya kufika robo fainali mara tatu hilo ndio linaloifanya timu hiyo kuogopwa.

Ingawa timu hiyo imekwenda bila kuwa na kocha mkuu baada ya Zoran Maki kuvunja mkataba siku mbili kabla ya safari ya Malawi, lakini hilo halionekani kuwa kikwazo kikubwa kutokana na ubora wa kikosi cha Simba na maandalizi waliyoyafanya ikiwemo kuweka kambini nchini Misri pamoja na kwenda Sudan kucheza mechi za kirafiki.

GEITA GOLD FC

Geita FC itacheza na Hilal Al Sahil ya Sudan ingawa timu hiyo inashiriki kwa kwa mara ya kwanza michuano hiyo lakini matumaini ya kufanya vizuri kwa wawakilishi hao wa Tanzania ni makubwa kutokana na maandalizi yao kuwa mazuri lakini pia ubora wa wachezaji iliyowaongeza kwenye dirisha kubwa la usajili.

Uwepo wa wachezaji wenye uzoefu akina Klevin Yonda, nahodha wake Danny Lyanga, George Mpole na wachezaji wengine wenye vipaji unatoa nafasi kwa timu hiyo kuonesha kwamba hawakupata nafasi hiyo kwa kubahatisha.

Kocha Mkuu wa Geita Fred Minziro siyo mgeni sana na michuano hiyo aliweza kushiriki akiwa na Yanga katika nafasi ya kocha msaidizi na amehudhuria mafunzo kadhaa ya ukocha hivyo kucheza na Hilal Al sahil inaweza kuwa ni sehemu ya kuthibitisha ubora waliokuwa nao kwake na taifa la Tanzania.

KMKM

Hii ni miamba ya soka kutoka Tanzania visiwani timu ambayo imeonesha utofauti mkubwa kiubora na timu nyingine za visiwani humo hawa wataanzia nyumbani uwanja wa Amaan dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ni mchezo mgumu lakini kwa maandalizi ya mabaharia hao bilashaka wapinzani watatoka vichwa chini.

Achana na ubora wa kikosi chao pamoja na usajili wa wachezaji mchanganyiko kutoka mataifa ya DR Congo na kwingineko lakini uzoefu wa kocha wao Hemed Seleman ‘Morocco’ ni miongoni mwa vitu vinavyo fanya timu hiyo kupewa nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata.

Morocco amethibitisha hilo msimu uliopita akiwa na timu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Zanzibar Heroes na hivi karibuni aliwafunga Uganda katika mchezo wa kirafikii.

KIPANGA FC

Hii ni timu kongwe ingawa ilipotea miaka ya karibuni timu hiyo imerudi kwa kasi na msimu uliopita ikafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho na ratiba ilionesha wataanzia ugenini lakini kutokana na machafuko nchini Sudani mchezo wao wa awali watacheza uwanja wa Uhuru Dar es Salaam dhidi ya Hilal FC Wau ya Sudan Kusini.

Kipanga haishiriki michuano hiyo kwa kubahatisha bali ilipambana na kuonesha ubora wake ndio maana ikapata nafasi hiyo na kutokana na maandalizi mazuri na usajili iliyofanya inapewa nafasi kubwa ya kwenda raundi ya kwanza hasa ukizingatia ubora wa mpinzani wake Hilal FC WAU siyo wa kutisha sana.

Related Articles

Back to top button