BurudaniFilamu

THE VEIL

POLISI wa nchini Korea Kusini wanapata taarifa za uwepo wa magendo katika pwani moja, ndani ya boti.

Operesheni nzito ya kikosi maalumu inagundua udhalimu mkubwa unaofanywa ndani ya boti hiyo dhidi ya binadamu wasio na hatia. Kwa kweli hali inatisha mno! Lakini wakati operesheni hii inaendelea polisi wanakutana na binadamu wa ajabu ambaye haoneshi kama ni mtu wa kawaida.

Uchakavu wa mwili wake unaonesha dhahiri kuwa kuna dhahama kubwa imemkuta. Swali ni; huyu mtu ni nani? Na imekuwaje yumo ndani ya boti hiyo?

Wanapotafuta taarifa zake inaonesha kuwa mwamba huyu ni mpelelezi wa usalama wa taifa (NIS), lakini pia ripoti zinaenda mbali kwa kuonesha kuwa alikufa mwaka mmoja uliopita! Sasa imekuaje yupo hai kama hii si hadithi ya kufikirika?

Tena katika hali hii mbaya! Kibaya zaidi ni kwamba mwamba huyu hakumbuki chochote! Sasa weka umakini wako katika kufuatilia uchambuzi huu ili uweze kujua nini kimejiri… Mwaka mmoja uliopita nchi ya Korea Kusini ilituma majasusi wake kwenda kufanya misheni katika nchi za Korea Kaskazini na China.

Operesheni hii (ya utatu) iliongozwa na Han Ji Hyuk, mmoja kati ya wapelelezi mahiri wanaotegemewa sana na kikosi cha NIS nchini Korea Kusini. Kwa kifupi ni kwamba Han Ji Hyuk yuko vizuri sana.

Mambo yalikwenda vizuri kwenye misheni yao hadi usiku mmoja wakiwa sehemu waliyofikia huko China wakahisi mambo hayako sawa. Han Ji Hyuk akainuka na kwenda kuona ni nini hasa kinaendelea. Na kama kuna mtu, ni nani?

Sasa kilichotokea baada ya kufungua mlango ndicho ambacho mwamba huyu hakikumbuki hadi leo na kinamtesa mno, kwa sababu baadaye ripoti zilitoka kuwa wenziwe wawili waliuawa kinyama pale pale wakati yeye mwili wake haukupatikana, na baadaye ikasemekana kuwa huenda na yeye aliuawa.

Ni nini kilitokea hadi wenziwe wakafa usiku huo, na yeye alikuwa wapi kwa mwaka mzima? Hili ndilo swali ambalo Han Ji Hyuk anajiuliza na leo anahitaji majibu. Lakini viongozi wake hawaoneshi kuwa wapo tayari kumpa majibu hayo. Kwa nini iwe hivi?

Ngoja tuone… Baada ya muda kidogo kupita na afya yake kutengemaa, leo anarudishwa tena kazini kujiunga na kikosi cha NIS ili maisha yaendelee, lakini bado moyoni mwake anataka kujua ni nini kilitokea usiku ule kule China, mwaka mmoja uliopita.

Wapelelezi wenziwe waliuawa na kwa nini yeye hakuuawa? Je, alipelekwa wapi? Kibaya zaidi kumbukumbu zake zinaishia pale tu alipokwenda kufungua mlango na kuwaacha wenziwe nyuma. Maswali ni mengi, baada ya kufungua mlango ni nani aliyemwona?

Ni nani aliyefanya mauaji hayo? Hayo ni mambo yanayomtesa kwa sababu hakumbuki. Mbaya zaidi kila anapojaribu kupiga hatua kutaka kuujua ukweli ofisi yake wanaonesha kuwa hawataki aujue ukweli, ni kama wanaomba kuwa kumbukumbu zake kuhusu tukio hilo zisimrudie.

Na jambo baya zaidi ni kwamba lawama za tukio hilo la mauaji anabebeshwa yeye, na bado hapewi ushirikiano wa kutaka kuujua ukweli. Kuna nini hapa kinaendelea?

Sasa leo kuna kitu anakiona kinamchomfanya kukumbuka jambo, anamwona kijana ambaye kumbukumbu zake zinamwambia kuwa ndiye aliyemfungulia mlango usiku ule.

Ndiyo! Huyu kijana walimtumia wakati wapo kwenye misheni yao nchini China ili kuwapatia baadhi ya taarifa. Sasa anakumbuka kuwa usiku huo huyu kijana alikuja kugonga na akamfungulia mlango. Sasa je, ni huyu kijana ndiye aliyefanya mauaji?

Na kama hajafanya basi atakuwa anajua nini kilitokea. Lakini kumbukumbu zaidi zinarudi na sasa anakumbuka kuwa kijana huyu hahusiki kwani alipomfungulia mlango waliishia kuongea tu kisha akaondoka zake na yeye kurudi ndani.

Dah, kumbe shida haipo tena pale kwenye kufungua mlango, inaonesha kuwa kuna mtu alikuja nyuma yake baada ya kuachana na kijana huyo. Sasa ni nani mtu huyo na kwa nini hakumbuki chochote?

Swali jingine ni kwa nini mtu huyo aliwaua wenzake na yeye alifanywa nini hadi kumbukumbu zake zipotee kwa zaidi ya mwaka mmoja? Anazidi kuchanganyikiwa kwani bado hana majibu.

Na kila anapofanya jitihada zake binafsi kutaka kuujua ukweli ofisi yake inaonesha kutofurahishwa na jambo hilo na hawataki afanye hivyo. Wanamtuliza. Kuna nini hapa? Sasa leo Han Ji Hyuk anaona kuwa huenda akapata mwanga na kuujua ukweli baada ya mvutano wa muda mrefu na wenziwe ofisini wakionekana kumficha ukweli.

Leo kuna mtu anajitokeza kumwambia ukweli wa kile ambacho kilitokea usiku ule. Huyu ni bibie Seo Soo Yeon, kiongozi mkuu wa idara ya habari za jinai ndani ya NIS. Huyu bibie alikuwa mchumba wa mmoja wa wapelelezi waliouawa kule kwenye misheni nchini China.

Seo Soo Yeon ameona ajilipue kwa kumwambia ukweli japo ni kama anasita hivi kwa sababu Han Ji Hyuk hapaswi kuujua ukweli huo, kwa gharama yoyote ile. Akiujua itakuwa shida.

Wakati Seo Soo Yeon anakaribia kumwambia ukweli anapigwa risasi. Dah! Mambo yanatibuka tena, na mbaya zaidi ni kwamba kamera za usalama zinaonesha kuwa muuaji ni yeye Han Ji Hyuk.

Lakini swali ni kwamba, anawezaje kumuua mtu aliyejitolea kumsaidia kuujua ukweli ili aweze kurudisha kumbukumbu zake?Sasa tena yeye ndiye anaonekana ameua? Mbona kama haiingii akilini?

Sasa anaanza kusakwa na taifa zima la Korea Kusini kama jasusi lililofanya mauaji dhidi ya mpelelezi wa usalama wa taifa, na hata wale waliouawa nchini China… Nisikuchoshe, itafute filamu hii ujionee kwani hii ni vita ya wababe na mtoto hatumwi dukani.

Ni filamu iliyotoka mwaka 2021 ikiwa imetengenezwa kwa bajeti ya dola za Marekani milioni 13.7.

Related Articles

Back to top button