World Cup

Tembo, Serengeti zachangiwa bil 1.27/-

WADAU wa michezo nchini wamechanga kiasi cha Sh bilioni 1.26 kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuzisaidia timu za Serengeti Girls na Tembo Warriors ili zishiriki vyema fainali za Kombe la Dunia nchini Uturuki na India.

Kikosi cha Tembo Warriors

Timu ya taifa ya soka la walemavu ya Tembo Warriors itashiriki fainali za 16 za Kombe la Dunia zitakazofanyika Uturuki Oktoba mwaka huu wakati ile ya Serengeti Girls itacheza fainali za Kombe la Dunia kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 nchini India Novemba mwaka huu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Samia katika kikao cha wadau cha kuchangisha fedha kwa ajili ya timu hizo mbili, ambazo zinahitaji kiasi cha Sh bilioni 3.76 kwa ajili ya maandalizi na fainali hizo.

Kikosi cha Serengeti Girls

Majaliwa ambaye aliongoza kikao hicho kwa kushirikiana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa alisema kuwa michango hiyo ya wadau inadhihirisha kuwa wanataka makombe ya dunia kuletwa nchini.

Mbali ya michango ya fedha, wadau hao waliahidi kulipia tiketi za safari kwa timu zote mbili, kulipia bima kwa wachezaji wa timu zote mbili, kutengeneza na kuzibrand jezi na suti za michezo, kununua viatu na soksi kwa timu hizo.

Aliwashukuru wadau wote kwa michango yao na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuthamini michango waliyoitoa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Michango hiyo imetolewa na wadau kutoka sekta za fedha/mabenki, mitandao ya simu, viwanda, taasisi za Serikali, vyombo vya habari, wadau binafsi na taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mchengerwa alisema ili timu hizo zipate maandalizi ya
kutosha zinahitajika Sh bilioni 3.76 ili kugharimia timu zote mbili, ambapo kati ya hizo, Serengeti Girls inahitaji Sh bilioni 2.57 na Tembo Warriors inahitaji Sh bilioni 1.19.

“Ili kujiandaa vizuri tumepanga kuzipeleka timu zote nje ya nchi kwa ajili ya kambi za mwisho kabla ya kuelekea kwenye mashindano hayo.”

Related Articles

Back to top button