Nyumbani

Tanzania kupokea ugeni wa viongozi wakuu CAF

Mkutano Mkubwa Kufanyika Dar

DAR ES SALAAM:TANZANIA inatarajia kupokea ugeni wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, anayekuja nchini kuongoza Mkutano wa Kamati Tendaji wa CAF, utakaofanyika Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema tayari maandalizi yamekamilika kupokea ugeni huo mkubwa, huku timu ya viongozi wa CAF ikitarajiwa kuanza kuwasili kuanzia Februari 10.

Makonda amesema mkutano huo utafanyika jijini Dar es Salaam na ni ishara ya imani kubwa ambayo Afrika imeiweka Tanzania, hususa katika sekta ya michezo, hasa mpira wa miguu.

“Hii ni habari njema kwa taifa letu. Ni fursa adhimu kwa Tanzania na ushahidi kuwa nchi yetu ni salama, ina miundombinu bora na ina mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo barani Afrika,” amesema Makonda.

Ameongeza kuwa uamuzi wa CAF kufanya mkutano wake Tanzania umetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Makonda ameeleza kuwa viongozi hao watapata fursa ya kujionea maendeleo makubwa ya miundombinu ya michezo nchini, hali itakayosaidia kutoa maamuzi chanya kuhusu mashindano na matukio makubwa ya kimataifa kufanyika Tanzania siku zijazo.

“Ugeni huu ni mafanikio makubwa kwa sekta ya michezo. Tunapata ushirikiano wa kitaalamu (technical support), kuimarisha mahusiano na kuhakikisha viwango vyote vya CAF vinatimia nchini,” amesema.

Amesema viongozi wa CAF watapokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Terminal 3, na baadaye kuelekea hotelini kupitia barabara kuu zilizoboreshwa, ikiwa ni ishara ya maandalizi makubwa na heshima kwa wageni hao.

Makonda amebainisha kuwa maandalizi ya ugeni huo yanafanywa kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ili kuhakikisha jiji linakuwa katika hali bora inayolingana na hadhi ya taifa.

Aidha, amesema katika mazungumzo yao na Rais wa CAF, Motsepe, waliwasilisha ujumbe maalum wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliotumwa Januari 16, 2026, ukitambua mchango wake mkubwa katika kuendeleza mpira wa miguu barani Afrika na kuimarisha amani kupitia michezo.

Makonda amesema Tanzania imeendelea kuwekeza zaidi ya Sh trilioni 1.76 katika ujenzi wa viwanja vipya Arusha, Dodoma na Dar es Salaam pamoja na miundombinu inayozunguka viwanja hivyo.

“Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya soka Afrika na ikiwezekana duniani,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Makonda, uamuzi wa CAF kufanya mkutano wake Tanzania ni ushahidi wa diplomasia madhubuti ya michezo na imani kubwa ya jumuiya ya mpira wa miguu Afrika kwa taifa la Tanzania.

Related Articles

Back to top button