Michezo Mingine

Tanzania kuandaa mkutano wa kihistoria wa wanachama wa ICC Kanda ya Afrika

DAR ES SALAAM: TANZANIA  imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wanachama wa Baraza la Kimataifa la Kriketi (ICC) Kanda ya Afrika kwa mwaka 2025.

Mkutano huo muhimu unafanyika jijini  Dar es salaam kuanzia Aprili 25 hadi 26 katika Hoteli ya White Sands, ukihusisha wadau wa kriketi kutoka zaidi ya mataifa 20 ya Afrika.

Kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania kupitia Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) itaandaa tukio hilo la kipekee, linalotarajiwa kuleta pamoja viongozi wakuu wa vyama vya kitaifa vya kriketi, marais wa mashirikisho, makatibu wakuu pamoja na maafisa waandamizi kutoka kote barani.

Akizungumza kuelekea mkutano huo, Mwenyekiti wa TCA, Dkt. Balakrishna Sreekumar, amesema  tukio hilo linaashiria hatua kubwa kwa taifa katika kukuza mchezo wa kriketi, huku likiwa jukwaa muhimu la majadiliano ya kimkakati, warsha na ushirikiano wa kuimarisha mchezo huo.

“Mkutano utafunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Wanachama Washirika wa ICC, Mubashshir Usmani, sambamba na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma. Pia Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Bi. Neema Msitha, atakuwepo kuonesha uungwaji mkono wa serikali,” amesema.

Dkt Sreekumar amebainisha  kuwa baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na maendeleo ya kriketi kwa vijana na wanawake, ujumuishaji, uboreshaji wa miundombinu, usimamizi bora, pamoja na mikakati ya kibiashara na kidigitali kwa ajili ya kuimarisha mchezo huo katika ngazi za shule na jamii.

“Tunajivunia kuwa wenyeji wa mkutano huu wa kihistoria. Hii ni fursa ya kipekee kuonesha dhamira ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla ya kukuza kriketi kupitia mshikamano, ubunifu na ushirikiano wa kweli,” ameongeza.

Kupitia mkutano huu, Tanzania si tu inajiimarisha katika ramani ya michezo ya kimataifa, bali pia inatoa fursa kwa maendeleo mapana ya kijamii na kiuchumi kupitia michezo

Related Articles

Back to top button