
INDIA: TAMASHA la msanii maarufu duniani, Shakira Mebarak maarufu Shakira, lililokuwa lifanyike nchini India limeahirishwa bila kutangazwa tarehe mpya kutokana na mvutano wa kisiasa na hali ya kijiografia, ikiwemo mgogoro kati ya Marekani na Iran.
Shakira, mshindi wa tuzo za Grammy, alikuwa amewapa mashabiki hamu kubwa baada ya kutangaza ziara yake ya kurejea India mwezi Aprili. Hata hivyo, taarifa ya kuahirishwa kwa tamasha hilo imewaacha mashabiki wengi wakiwa na huzuni na maswali mengi.
Waandaaji wa tamasha hilo, kupitia jukwaa la District, walitangaza kwenye mitandao ya kijamii wakisema:
“Kutokana na hali ya sasa ya kisiasa na mvutano wa kikanda, tamasha la ‘Feeding India Concert’ linalomshirikisha Shakira limeahirishwa hadi itakapotangazwa vinginevyo. Usalama wa mashabiki, msanii na timu ya uzalishaji ni kipaumbele chetu.”
Aidha, waandaaji wameeleza kuwa wanatafuta tarehe mpya za tamasha hilo, huku wakiahidi kurejesha fedha zote za tiketi kwa mashabiki kupitia njia walizotumia kulipia ndani ya siku 5 hadi 7 za kazi.
Licha ya hilo, mashabiki wengi wameonesha kutoridhishwa na uamuzi huo, wakitaka kufahamu kama gharama nyingine walizotumia kama tiketi za ndege na malazi pia zitarejeshwa. Wengine walieleza wazi masikitiko yao wakisema walikuwa wanasubiri kwa hamu kubwa tukio hilo.
Kabla ya tukio hili, msanii Kanye West pia alilazimika kuahirisha tamasha lake nchini India kwa miezi miwili kutokana na mvutano huo huo, ambapo sasa linatarajiwa kufanyika mwezi Mei badala ya Machi.
Tamasha la Shakira lilipangwa kufanyika Aprili 10 na 11 jijini Mumbai na Aprili 15 jijini Delhi, likiwa sehemu ya mpango wa kijamii wa ‘Feeding India’ kwa kushirikiana na District by Zomato. Hii ingekuwa ni onesho lake kubwa la kwanza nchini India baada ya takribani miaka 19 tangu alipofanya tamasha lake la mwisho mwaka 2007 jijini Mumbai




