CHAN

Sudan yatamba kutusua, yasifu mapokezi Zanzibar

ZANZIBAR: KOCHA Mkuu wa Sudan, Kwesi Appiah, amesema licha ya kuanza michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kwa kusuasua wakiwa hawana maandalizi mazuri wanashukuru wamesonga mbele hatua ya robo fainali.

Sudan maarufu kama The Falcons of Jediane imefuzu robo fainali ya michuano ya CHAN 2024, ikiwa kinara wa Kundi D. Waliibuka vinara kwa tofauti ya mabao dhidi ya mabingwa watetezi Senegal baada ya sare ya bila kufungana usiku wa Jumanne Zanzibar.

Cha kushangaza, kikosi hicho cha Sudan kilikusanyika siku nne tu kabla ya kuanza kwa mashindano, lakini kimefanikiwa kuibuka kikiwa hakijapoteza mchezo wowote hatua ya makundi.

“Tulianza mashindano kwa kusuasua lakini tukapiga hatua, tukawashinda Nigeria na kupata matokeo mazuri dhidi ya Senegal. Kadri tunavyosonga mbele, ndivyo tunavyokuwa bora zaidi,” alisema Appiah, kocha wa zamani wa Ghana.

Sudan ilianza kwa sare ya 1-1 na Kongo, ikiruhusu bao la dakika za mwisho, lakini tangu hapo imeonesha ubabe kwa kuichapa Nigeria mabao 4-0 na kisha kulazimisha sare dhidi ya Senegal.

Akizungumzia mechi ya mwisho ya kundi, Appiah alikiri kuwa alitumia mbinu ya kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza.

“Senegal si nchi ndogo kisoka. Tulijua ni mchezo mgumu, tukakaa nyuma na kutumia mashambulizi ya kushtukiza. Tulicheza vizuri na kuwapunguza kasi washambuliaji wao,” alisema.

Appiah pia alisifu mapokezi ya Zanzibar, akisema yameongeza morali ya kikosi chake. “Watu wa Zanzibar wamekuwa wa kipekee. Hawatakiwi kuvunjwa moyo na ubora wa soka letu. Wamekuwa na mshikamano nasi, hata lugha inatufanya tuwe karibu,” alisema.

Sudan sasa itakutana na Algeria, washindi wa pili wa CHAN 2022, kwenye robo fainali

Related Articles

Back to top button