Kwingineko

Steve Nyerere awajia juu waliomzushia kifo

DAR ES SALAAM: MSANII na mchekeshaji maarufu nchini, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, amesema bado yuko hai na kuwataka watu kupuuza taarifa zilizozuka mitandaoni leo kuwa amefariki dunia.

Steve aliweka taarifa inayosambaa kwenye mtandao wa TikTok kuwa amefariki jambo ambalo sio kweli.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Steve Nyerere amesema bado yuko hai na mwenye afya njema, akiwataka mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa hizo ambazo amezitaja kuwa za kipuuzi na zisizo na msingi wowote.

“Mstafuuu… ni ujinga na utoto, kukosa maarifa. Mimi ni mzima wa afya, nipo. Naomba muwapuuze wapuuzi,” aliandika Steve ambaye pia, ni Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea na Mwanao.

Ameongeza kuwa taarifa hizo za kuzushiwa kifo zimezua taharuki kubwa kwa watu wake wa karibu, huku simu kutoka kwa marafiki na familia zikimiminika kila kona kwa hofu na mshangao.

“Kila kona naona simu zinaita. Napenda kusema ni matumizi mabaya ya mitandao yanayotumiwa na vikundi vya hovyo kusababisha taharuki. Nilikuwa sijui kama nimekufa,”aliongeza.

Steve Nyerere ambaye amekuwa akijipambanua pia kama mwanaharakati wa masuala ya kijamii na kisiasa, amesema hali kama hii inapaswa kukemewa kwa nguvu zote na mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya watu wanaosambaza taarifa za uongo kwa makusudi.

Tukio hili limeibua mjadala mpana mitandaoni kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, huku wengi wakimtumia jumbe za faraja na kumtakia afya njema Steve Nyerere, ambaye bado anaendelea na shughuli zake kama kawaida.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button