Stand United yapokwa pointi tatu

DAR ES SALAAM: KLABU ya Stand United ya mkoani Shinyanga imepoteza mchezo dhidi ya timu ya Hausung FC ya Njombe kwa kosa la kushindwa kufika uwanja wa Amani bila sababu za msingi na zinazokubalika na hivyo, kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kufuatia tukio hilo Hausung FC imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) .
Sambamba na adhabu hiyo, Stand United imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi), na kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.
Pia, Mwenyekiti wa klabu ya Stand United, Stivian Antitius amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani.
Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship kuhusu Kutofika Uwanjani.



