Spurs yaifilisi Brentford benchi la ufundi

LONDON, Mabingwa wa Europa League Tottenham Hotspur wamemtangaza aliyekuwa kocha wa Brentford Thomas Frank kuwa kocha wao mkuu mpya kurithi mikoba ya Ange Postecoglou aliyetimuliwa hivi majuzi kwa mkataba utakayodumu hadi mwisho wa msimu wa 2027/2028.
Kocha huyo mwenye miaka 51 anawasili Spurs kutoka Brentford, ambako alikaa kwa miaka saba, akiwaongoza Nyuki hao kupanda Ligi Kuu mwaka 2021, akiwa mtu wa kwanza kuwaongoza kufanya hivyo tangu klabu hiyo ilipocheza ligi kuu msimu wa 1946/47.
Wadau wa soka nchini England wanasema Spurs imelamba dume kwani tangu wakati huo Frank ameimarisha hadhi ya Brentford kwenye EPL na nafasi ya 10 waliyomaliza msimu uliopita inafanya klabu hiyo kumaliza kwenye nusu ya kwanza ya jedwali la msimamo wa ligi mara ya pili ndani ya miaka minne.
Katika taarifa ya kumuaga iliyopo kwenye tovuti ya klabu, Brentford imesema haitamsahau kocha huyo kwa nyakati zote nzuri na mbaya walizokuwa Pamoja huku ikimtaja kama mtu maalum aliyejitolea asilimia 100 kwenye kazi na kumtakia kila la heri kwenye majukumu mapya.
Frank anachukua mikoba ya kuinoa Spurs baada ya msimu mbaya chini ya Muaustralia Ange Postecoglou Spurs ikimaliza katika nafasi ya 17 nafasi yao ya chini zaidi kuwahi kumaliza baada ya kupoteza mechi 22 kati ya 38 za Premier League.
Frank ataifundisha Tottenham na timu ya wakufunzi alioondoka nao Brentford kama kocha wake msaidizi Justin Cochrane, ‘perfomance coach’ na kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza Chris Haslam na Joe Newton ambaye ni ‘analyst’ wa kocha wa kikosi cha kwanza huku kutoka Manchester Utd kocha msaidizi Andreas Georgson aatajiunga nae.




