Son aacha maswali Spurs

SEOUL:NAHODHA wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Korea kusini Son Heung-min amezua mjadala juu ya mustakabali wake katika klabu hiyo baada ya kusema “atasubiri na kuona” kitakachotokea alipoulizwa ikiwa atasalia Spurs baada ya kuwa na tetesi kwamba nahodha huyo anaweza kuhamia Saudi Arabia.
Mshambuliaji huyo wa Korea Kusini amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Tottenham na amekuwa akihusishwa na kutimkia kunako moja ya klabu za Saudi Arabia zinazoshiriki ligi kuu ya Saudi Pro League siku chache baada ya kuisaidia klabu hiyo kumaliza ukame wa miaka 17 kwa kutwaa taji la Europa League mele ya United.
“Badala ya kusema lolote kwa wakati huu, nadhani sote tunapaswa kusubiri na kuona kitakachotokea, Lakini haijalishi nitaangukia wapi, nitafanya kila niwezalo kuwa bora zaidi ya nitakapotoka. Hilo halitabadilika kamwe.” Son aliwaambia waandishi wa habari baada ya ushindi wa 4-0 wa Korea Kusini katika michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Kuwait siku ya Jumanne.
Son alinyanyua taji la Europa League mwezi uliopita likiwa taji lake la kwanza akiwa na Tottenham baada ya kuisaidia timu yake kuishinda Manchester United 1-0 mjini Bilbao.
Spurs tayari wamemtimua kocha Ange Postecoglou kufuatia mwenendo mbaya kwenye Ligi kuu iliyowafanya kumaliza nafasi moja juu ya eneo la kushuka daraja. Son alikumbana na hasira ya mashabiki baada ya kuonesha kiwango duni lakini ameapa kurejea kwa nguvu zaidi msimu ujao, popote atakapokuwa.