Featured

Soka lilivyochomoza kimataifa 2022

MWAKA 2022 ndio unaelekea ukingoni huku ukiacha matukio mengi mazuri na mabaya yaliyotokea kwa kipindi cha miezi 12.

Kwa kipindi cha miezi 12 mchezo wa soka umeitangaza Tanzania kimataifa na kufanya watu wengi kuifahamu nchi hii ya Afrika Mashariki.

Kupitia soka timu ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls ilishiriki fainali za Kombe la Dunia nchini India na timu ya walemavu ya mpira wa miguu ilishiriki Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Uturuki.

Aidha, Simba Queens ilishiriki fainali za soka la wanawake Afrika na kushika nafasi ya nne na Simba na Yanga zimefuzu makundi ya mashindano ya kimataifa Afrika.

Serengeti Girls

Oktoba mwaka huu timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls  ilicheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake zilizofanyika nchini India kuanzia Oktoba 11 hadi 30.

Maendeleo ya juu kabisa kufikiwa katika mpira wa miguu kwa Tanzania kuwa na mwakilishi katika fainali hizo za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizoshirikisha timu 16 kutoka katika mabara yote duniani.

Tanzania ilikuwa moja kati ya nchi tatu zilizoiwakilisha Afrika, timu nyingine kutoka Afrika zilikuwa ni Nigeria na Morocco.

Uwakilishi wa timu hizi kwa Afrika ulikuwa mzuri, kwani wakati Morocco ikitolewa katika hatua ya makundi Tanzania ilicheza robo fainali na Nigeria ilifika hatua ya nusu fainali na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Katika fainali hizo, Tanzania na Nigeria zote zilitolewa na Colombia ambayo ilishika nafasi ya pili na Hispania ikifanikiwa kutetea ubingwa wake tena. Kwa hatua ambayo Serengeti Girls imefikia, inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa timu 16 bora duniani kwa mpira wa miguu wa wanawake kwa umri chini ya miaka 17.

Serengeti Girls ilikuwa katika Kundi D pamoja na timu za Japan, Ufaransa na Canada na iliwavutia wengi kwani wachezaji zaidi ya sita waliwavutia mawakala mbalimbali na baadaye wakifikisha miaka 18 watakuwa na nafasi ya kwenda kucheza soka Ulaya na sehemu nyingine ambapo kisheria ndipo wanaweza kusaini mikataba ya ajira.

Tembo Warriors

Kwa kuonesha kuwa Tanzania inaheshimu usawa na kuwapa nafasi ya kucheza timu ya
walemavu ya mpira wa miguu ilishiriki Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Uturuki kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 5 mwaka huu.

Tembo Warriors ambayo iliwakilisha Bara la Afrika pamoja na Liberia, Morocco na Angola walifanikiwa kufika hatua ya robo fainali. Morocco nayo iliishia nusu fainali wakati Angola ilicheza fainali na wenyeji Uturuki.

Kwa Tembo Warriors kufika robo fainali ni mafanikio makubwa kwani ni mara ya kwanza kushiriki fainali hizo na tena ikiwa timu changa ambayo ina miaka minne tangu kuanzishwa kwake.

Simba na Yanga
Kwa upande wa klabu ya Simba imefanya vizuri katika vipindi mbalimbali na kufanikiwa kuiwezesha Tanzania kuwa na wawakilishi wanne katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Simba imefanikiwa kufika robo fainali hatua ambayo imeifanya kuwa miongoni mwa timu zinazoogopwa katika mashindano ya Caf na safari hii imefanikiwa kutinga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa.

Pia klabu ya Yanga nayo inafanya vizuri na imetinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho.

Simba Queens

Simba Queens ambayo ni bingwa wa Ligi ya Wanawake Tanzania Bara kwa misimu mitatu mwaka huu ilishiriki fainali za wanawake Afrika zilizofanyika nchini Morocco na kufanikiwa kushika nafasi ya nne.

Kitendo cha Simba Queens kupenya ikiwa ni timu pekee kutoka Ukanda wa Cecafa ni maendeleo ya kukua kwa soka la wanawake. Msimu wa mwaka jana, Simba Queens ilishiriki fainali hizo lakini haikufanya vizuri kwani iliishia kwenye hatua ya awali.

Soka la wanawake kwa Tanzania limekuwa la kuigwa kwani limeifanya Tanzania kujulikana na pengine kuwa miongoni mwa timu za kuogopwa zinakutana na wapinzani wengine.
Pamoja na maendeleo yaliyopo katika soka la wanawake bado jitihada zaidi zinahitajika ili kuendelea kupaisha soka zaidi na zaidi.

Thamani iliyooneshwa na Serengeti Girls na Simba Queens inahitajika kuendelezwa zaidi ili Tanzania iendelee kuwa kinara kwa upande wa Afrika na duniani.

Related Articles

Back to top button