Slot anena mazito Liverpool ikitakata ugenini

FRANKFURT: USHINDI mnono wa mabao 5–1 wa Liverpool dhidi ya klabu ya Bundesliga Eintracht Frankfurt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya umevunja mfululizo wa michezo minne bila ushindi, huku pia ukitoa ishara ya muunganiko hatari wa washambuliaji wa klabu hiyo kama majeraha hayataingilia kati.
Ingizo jipya Hugo Ekitike, aliyeanza kwa mara ya kwanza sambamba na Alexander Isak, alifunga bao la kwanza la Liverpool, huku Isak ambaye alikosa ‘Pre-season’ kutokana na Sakata la usajili wake kuchukua mrefu akiondoka uwanjani muda cha mapumziko kutokana na majeraha ya nyonga.
“Tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi za kufunga siku za karibuni lakini tumeshindwa kuzitumia. Leo, kwa kuwa na Alex na Hugo, nilikuwa na wachezaji wawili ambao kwa kawaida wana uwezo wa kufunga. Wote wawili wamefanya kile nilichotarajia mikimbio yao nyuma ya safu ya ulinzi, ilikuwa tishio kwa wapinzani, na walifanya vizuri.” – amesema kocha wa Liverpool Arne Slot
“Alex alikaribia kufunga mara kadhaa, lakini ilibidi atolewe kipindi cha kwanza. Hapo ndipo changamoto ilipo. Hakuwa amefanya mazoezi ya kutosha kabla ya kujiunga nasi, na tumekuwa tukimjenga hatua kwa hatua. Nahisi kuna wakati atakuwa tayari kucheza mara mbili kwa wiki, lakini jaribio la kwanza tu, analazimika kutoka. Tumaini letu ni kwamba jeraha si kubwa.” – aliongeza
Slot alibainisha kuwa Isak alicheza mara mbili kwa timu ya taifa ya Sweden wakati wa mapumziko ya kimataifa, licha ya klabu kuwafahamisha viongozi wa timu hiyo kuwa hakuwa katika hali nzuri ya kucheza.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuna changamoto za kumjumuisha mshambuliaji huyo katika kikosi, hasa kutokana na ratiba ngumu ya timu hiyo.
“Ikiwa wewe ni Liverpool, unacheza kila baada ya siku tatu. Tumecheza mechi tatu ndani ya siku saba msimu huu, jambo ambalo ni gumu hasa bila maandalizi ya kutosha ya kabla ya msimu.” alisema Slot.