Slot aitamani ‘Top four’ ya EPL

LIVERPOOL: Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amesema kikosi chake kiko katika hali mbaya na kinalazimika kupambana kurejea kwenye ‘Top Four’ ya Ligi Kuu England, baada ya kushinda mechi mbili pekee kati ya tisa zilizopita.
Liverpool wanaendelea kusota katika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 22 kutokana na mechi 14, wakiachwa kwa pointi 11 na vinara Arsenal, licha ya kutumia pauni milioni 446 kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Leeds United, Slot amesema lengo lao la kwanza ni kurejea kwenye nafasi nne za juu kisha ataanza kuwaza kutetea Ubingwa.
“Ndio malengo yetu makuu kurejea kwenye ‘top four’ kwa sababu hatujaridhishwa na nafasi tulipo kwa sasa, najua sio rahisi hasa tukiwatazama wenzetu lakini ni lazima tufanye” – amesema.

Pamoja na matokeo yasiyoridhisha, kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya wachezaji wapya kama Florian Wirtz, Milos Kerkez, na Alexander Isak.
“Kuna mambo mazuri kutoka kwa wachezaji tuliowasajili majira ya kiangazi. Florian anaonekana zaidi, lakini ninaona maendeleo kama hayo kwa Milos pia. Alex alipata bao lake la kwanza mechi moja iliyopita, hivyo kuna vitu vizuri, ingawa bado hatujafika tunakotaka.” Amesema Slot
Kiwango cha sasa cha Mohamed Salah, ambaye amefunga mabao matano katika mechi 19 msimu huu, kimekuwa gumzo baada ya kuanza benchi kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya West Ham United na pia kutokea benchi katika sare ya 1-1 na Sunderland. Slot amesisitiza kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 bado ni sehemu muhimu ya mpango wake.




