“Slot aiokoe Liverpool mapema” – Gerrard

LIVERPOOL: ALIYEKUWA nahodha wa Liverpool Steven Gerrard, amesema Kocha Arne Slot, wa klabu hiyo ni lazima atafute mbinu mpya za kusitisha mwendo mbaya wa klabu hiyo huku presha ikizidi kupanda juu ya mustakabali wake klabuni hapo baada ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa PSV Eindhoven kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano.
Kipigo hicho cha aibu ni cha tisa kwa Liverpool katika mechi 12 zilizopita kwenye mashindano yote rekodi mbovu zaidi ya mechi 12 tangu msimu wa 1953/54 na ni mechi ya tatu mfululizo kupoteza kwa tofauti ya mabao matatu.
Slot aliisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa Premier League katika msimu wake wa kwanza, lakini sasa timu hiyo imeporomoka hadi nafasi ya 12 kwenye ligi na ya 13 kwenye Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, Gerrard amepuuza madai kuwa klabu iko kwenye mgogoro wa aina yeyote.

“‘Crisis’ ni neno kubwa, pia ni kukosa heshima kwa baadhi ya wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa klabu hii, na kwa kocha aliyeleta mafanikio miezi mitatu tu iliyopita,” – Gerrard, aliyecheza mechi 710 Liverpool, ameiambia TNT Sports.
“Lakini huwezi kukataa kuwa timu inateseka sana, wako kwenye mwenendo mbaya, hali ya kujiamini iko chini kabisa na wanaendelea kudidimia. Lazima kocha apate majibu na uthabiti ndani ya kikosi haraka.”
Kwa Upande wake Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya England na Liverpool, Steve McManaman, anaamini mazungumzo kuhusu hatma ya Slot ni ya mapema mno na anapaswa kupewa muda zaidi.
“Nadhani ni mapema sana kuuliza maswali hayo. Ni mpaka watolewe Ligi ya Mabingwa na wawe wanadidimia karibu na mkia wa EPL hapo ndipo maswali yatafaa kuanza kuulizwa. Wanacheza na Arsenal wiki ya pili ya Januari, hapo ndipo swali la hatma yake linaweza kuulizwa. Watakuwa nusu ya msimu kufikia wakati huo.”
Liverpool watakuwa ugenini dhidi ya West Ham United Jumapili kwenye Premier League.




