Siri ya kutinga makundi ni jitihada na dhamira-Arafat

MAKAMU wa Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Haji amesema siri ya timu hiyo kutinga hatua ya makundi ni jitihada na dhamira za wachezaji katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain uliochezwa Novemba 9 mjini Tunis, Tunisia.
Akizungumza na SpotiLeo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) Dar es Salaam leo baada ya timu hiyo kuwasili Arafat amesema baada ya kupata suluhu nyumbani waliweka mkakati maalumu ikiwemo kuwatimizia wachezaji mahitaji yote muhimu ili kushinda mchezo huo.
“Nawashukuru wachezaji kwa juhudi zao lakini pia benchi la ufundi kwa kazi kubwa walioifanya kuwapa wachezaji mbinu mbadala zilizowezesha kupata ushindi,” amesema Arafat.
Amesema mapambano yataendelea mechi zijazo za hatua ya makundi sababu lengo ni kucheza fainali za mashindano hayo mwaka huu.
Baada ya kuwasili Yanga itaondoka leo usiku kuelekea Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Kirumba Novemba 13.